ASKOFU Msaidizi wa
Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, amekiri
kupokea sh.milioni 40.4 alizoingiziwa katika akaunti yake kwenye Benki
ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa hilo kutoka kwa Kampuni ya VIP
inayomilikiwa na Kanisa hilo kutoka kwa Kampuni ya VIP Engineering and
Marketing ambayo inamilikiwa na Bw. James Rugemalira.
Alisema fedha hizo ziliingizwa katika akaunti hiyo Februari 2014, baada ya Bw.Rugemalira kumuomba namba ya akaunti yake ili aweze kuweka matoleo yake yaweze kusaidia katika shughuli za kitume na kichungaji.
Askofu Nzigilwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari tangu atajwe kwenye Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa miongoni mwa viongozi wa dini na watu wengine waliopokea mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Viongozi wengine wa dini waliotajwa katika ripoti hiyo ni Askofu Msaidizi wa Kanisa hilo, Jimbo la Bukoba, mkoani Kagera, Methodius Kilaini ambaye naye alikiri kupokea sh. milioni 80.5 kutoka kwa Bw.Rugemalira na kusema fedha hizo alizipokea kwa ajili ya miradi mbalimbali inayoendeshwa na kanisa.
“Nilipokea matoleo hayo kwa moyo mkunjufu kutoka kwa mtu anayefahamika kwa ukarimu alionao wa kusaidia kanisa, watumishi wake, kampuni anayomiliki na biashara anazofanya Bw.Rugemalira kwa mujibu wa sheria za nchi, haviwezi kumpa mashaka mtu anayemfahamu kuhusu uwezo wake au kampuni yake kutoa mchango mkubwa kama huo.
“Ni desturi na kawaida kwa waumini wa kanisa kutoa michango na matoleo mbalimbali kadiri ya uwezo na ukarimu wao, matoleo ya waumini hutumika katika shunguli za uinjilishaji, uendeshaji majimbo, Parokia na taasisi, pia hutumika katika miradi maalumu iliyokusudiwa na matoleo hayo au kwa matakwa na malengo ya mtoaji,” alisema.
Askofu Nzigilwa alisema, tangu Bw.Rugemalira atoe matoleo hayo, hakuna mamlaka iliyowahi kumuuliza kuhusu jambo hilo hivyo aliwaomba waumini kuendelea kujitoa kwa hali na mali ili kulijenga kanisa la Mungu.
“Kila aliyepewa talanta na Mungu, aitumie kuzalisha matunda mema ili kulijenga kanisa letu tuweze kuurithi ufalme wa Mbinguni, kanisa litaendelea kuwa mstari wa mbele kutetea haki, ukweli na
uadilifu na halitarudi nyuma wala kukaa kimya katika kukemea maovu kwenye jamii,” alisema Askofu Nzigilwa.
Alisema Bw. Rugemalira na familia yake ni waumini Wakatoliki katika Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozari Mtakatifu, Makongo Juu, Jimbo Kuu la Dar es Salaam pia ni washiriki wazuri katika ibada za Parokia, wenye moyo wa ukarimu katika kuchangia shughuli mbalimbali za kanisa.
Ripoti ya PAC mbali ya kumtaja Askofu Nzigilwa na Askofu Kilaini, pia ilimtaja Padri Alphonce Twimanye Simon na kudai alipokea sh. milioni 40.4 kutoka katika akaunti hiyo.
Chanzo:Majiraa
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment