Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil.
Katika uchunguzi wake, kamati hiyo ilibaini kuwa walioitwa katika
ajira hizo walikuwa ni ndugu na jamaa za maafisa wa idara hiyo.
Hata hivyo, akizungumza na NIPASHE jijini Dar es Salaam jana,
Msemaji wa wizara hiyo, Isaac Nantanga, alisema kuwa watumishi hao
wameshindwa kuchukuliwa hatua kwa kuwa hakuna ushahidi wa wazi
uliopatikana kuthibitisha tuhuma za upendeleo zilizoelekezwa kwao.
Alisema ndugu na jamaa za maafisa hao walikuwa na sifa za kuajiriwa
ndani ya idara hiyo na hivyo, kukosekana kigezo cha kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, alisema Wizara ilitoa onyo dhidi ya waliohusika na
mchakato huo kutokana na kutoa mwanya wa kuzuka malalamiko kutoka kwa
wananchi kuhusiana na ajira hizo.
“Waliitwa kazini, walistahili kuajiriwa, kwani walikuwa na sifa.
Pia walistahili kuomba mara ya pili, maombi hayakubagua, bali
zilizingatiwa sifa tu,” alisema Nantanga.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa malalamiko ya kuajiriwa ndugu na jamaa
za maafisa hao hayakuwa na msingi wowote na kwamba, onyo la wizara
limelenga kuwatahadharisha waliohusika na mchakato huo ili tukio kama
hilo lisijirudie tena ndani ya idara hiyo.
Alisema watumishi wa umma nao pia wanalindwa na sheria ya ajira,
hivyo, hawawezi kufukuzwa kazi kwa kutuhumiwa tu, lazima uthibisho
uwasilishwe na mamlaka husika zijiridhishe.
Agosti 22, mwaka jana, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak
Abdulwakil, alizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na
kusema baada ya waombaji wa nafasi hizo kufanyiwa usaili na kuitwa
kazini, ziliibuka tuhuma mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii.
Tuhuma hizo zilihusu upendeleo wa ajira kwa ndugu na jamaa za
watumishi wa idara hiyo, hivyo wizara ililazimika kuzisitisha na kuunda
kamati ndogo ya watu watano ili kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai
hayo.
Kamati hiyo ilipewa siku 10, kuanzia Agosti mosi, mwaka jana
kukamilisha kazi hiyo, ambayo waliifanya kwa muda waliopewa na kutoa
matokeo.
“Katika uchunguzi wao, kamati imebaini kuwa baadhi ya wasailiwa
waliolalamikiwa wamethibitika kuwa ni watoto wa ndugu au jamaa wa
watumishi wa idara hii.
“Baadhi ya waombaji wa nafasi hizi, walikuwa na umri mkubwa zaidi
ya ule uliotajwa kwenye matangazo ya kazi (Konstebo miaka 25 na Koplo
miaka 30), lakini walisailiwa na kuitwa kazini,” alisema Abdulwakil.
Alisema baadhi ya wasailiwa waliopata alama za juu katika ufaulu
hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalumu, ambazo zimetolewa, matangazo
ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari, yalikuwa ya jumla na
hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha
nne na sita.
Abdulwakil alisema kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, ajira hizo zimefutwa na zitatangazwa upya.
Awali, ajira hizo zilitangazwa na Kamishna wa Uhamiaji katika
Gazeti la Serikali, Februari 17, mwaka jana na kutoa tangazo hilo kwenye
tovuti ya wizara na idara ya Uhamiaji.
Baada ya kutangazwa ajira hizo, maombi 15,707 yalipokelewa na
waombaji 1,005 waliitwa katika usaili. Kati yao, 200 walishinda na
kuitwa kazini, lakini baada ya kutoa tangazo la kuitwa kazini,
malalamiko yalitolewa kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii
kuwa walioitwa katika ajira hizi ni watoto wa jamaa na ndugu.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment