Lile sakata la kushushwa kwa bei za filamu, limeingia katika
sura mpya baada ya watayarishaji wa filamu nchini kujitokeza na kutoa
malalamiko yao kwa Bodi ya Filamu, kuhusu kutoshirikishwa katika vikao
vinavyoendelea.
Bodi ya Filamu kwa kushirikiana na Wizara ya
Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Wizara ya Fedha na Wizara ya
Viwanda na Biashara, TRA, TBS, imekuwa ikifanya vikao vya ndani zaidi ya
viwili sasa na wasambazaji wa filamu ili kuzungumzia suala ya bei ya
filamu.
Mtayarishaji wa filamu Mike Sangu aliliambia
Mwananchi kuwa kitendo cha bodi hiyo kuendesha kikao pasipo wao
kushirikishwa, kimewaumiza na kwamba wanahitaji haki itendeke ili
biashara ya filamu isonge mbele kwa manufaa.
“Tunaiomba serikali kupitia vyombo vyake vyote
vinavyoshiriki haya masuala ya filamu, kusifanyike mkutano wa aina
yoyote ile kuzungumzia bei ya filamu bila kushirikisha maprodyuza, sisi
ndiyo wenye filamu na ndiyo tunaotengeneza sasa iweje tusishirikishwe,”
alisema Sangu na kuongeza:
“Inashangaza ikiwa msambazaji atapanga yeye bei,
badala ya sisi ambao ndiyo wazalishaji, kwa sababu tungeweza kusambaza
wenyewe, lakini tunawauzia wao ili wafanye biashara, hivyo lazima na
sisi tujue nini kinaendelea, kikao cha pili tulipata taarifa juu juu
kupitia watu tuliamua kuhudhuria ili kujua bei wanazopanga na sisi
tuwauzie kwa bei gani, badala yake tulifukuzwa na kikao kikavunjika.”
Mwongozaji na mtayarishaji filamu Chiki Mchoma
naye alisema kumekuwa na upotoshaji kwamba msambazaji mkubwa ndiye
aliyeamua kushusha bei ya filamu, lakini wao ndiyo waliomtaka afanye
hivyo.
“Kuna mkanganyiko wa bei kutoka kwa msambazaji
mpaka kwa mlaji ndiyo umesababisha migogoro hii, ilianzia kwetu baada ya
kuona hali halisi ya mfumo wa bei ya filamu bado haukui, soko linazidi
kuyumba tuligundua kwamba wizi wa filamu umekuwa ndiyo mtihani wetu,
tukaona kuna kila sababu ya kuhakikisha tunaudhibiti, tulimuomba
msambazaji mkuu ambaye ni Steps Entertainment kuhakikisha kwamba
anatafuta mbinu mbadala,” alisema Mchoma.
Alipoulizwa kuhusu sakata hilo, Katibu Mtendaji wa
Bodi ya Filamu na Ukaguzi wa Michezo ya Kuigiza Tanzania, Joyce Fisoo
alisema hawajawatenga watayarishaji, bali walizingatia upande mmoja
kwanza kwa kukaa na wasambazaji ili maamuzi yatakayofikiwa wayatangaze
kwa wasanii wote kwa ujumla.
“Tunapoendesha vikao vinavyohusu masuala ya
filamu, huwa tunafanya kwa makundi, sasa suala linalowahusu wasambazaji,
hatuwezi kukaa na watayarishaji lazima tutashindwa kufikia muafaka,
sisi hatubagui mtu bali kila mwana tasnia huwa tunakutana naye na
kuzungumza naye,” alisema Joyce.
Alisema suala la kibiashara limewafanya wazungumze
na wafanya biashara ambao ni wasambazaji, bali watayarishaji nao
wangeshirikishwa baadaye.
“Kikao cha wiki jana tulikaa na Wizara ya Habari,
Utamaduni na Michezo, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara,
TBS, TRA, Cosota na wengineo ili kufikia muafaka. Kikao cha juzi
hakikuwa cha kupanga bei bali kilihusu maadhimio ya kikao kilichofanyika
Desemba 30 mwaka jana,” alisema Joyce.
Alisisitiza kuwa watayarishaji bado wana nafasi
yao na wataitwa ili kutoa ushauri wa nini kifanyike kuhusu sakata hilo,
kwani serikali ilihitaji kupata taarifa kutoka upande wa wasambazaji
kwanza.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment