Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye.
Hali hiyo inatokana na kuendelea kutanda kwa kimya kizito kutoka
kwa mamlaka za ndani ya chama hicho tawala zinazoshughulikia maadili.
Makada wengine waliofungiwa kwa takribani mwaka mmoja sasa kutokana
na kosa hilo ni Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Mbunge wa Jimbo
la Sengerema, William Ngeleja, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, Januari Makamba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika,
Stephen Wasira.
Jana NIPASHE ilimtafuta Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho,
Nape Nnauye ili azungumzie suala hilo, lakini alieleza kwa kifupi tu
kwamba, "taarifa kuhusiana na hatua zitakazochukuliwa juu ya suala hilo
itatolewa".
Nape ambaye hakuweka wazi endapo adhabu ya makada hao imefikia
ukomo au laa, alisema Kamati Kuu ya CCM ndiyo itatoa maamuzi juu ya
matokeo ya utekelezaji wa adhabu kwa makada hao baada ya kupelekewa
ripoti kutoka kwa baraza la maadili la chama hicho ambalo ndilo lenye
mamlaka ya kuthamini utekelezaji wa adhabu zao.
“Mara kadhaa mmeniuliza swali hili, CCM tunasema hivi, muda
ukiisha taarifa mtapewa... kujua kama adhabu yao imeisha au laa. Na
kamati itakaa lini, hiyo siyo kazi yenu. Na mimi mwenyewe sijui kwa
sababu kazi ya kutathmini adhabu za watu hao haiko katika ofisi yangu.
Inafanywa na taasisi nyingine ndani ya chama,” alisema na kuongeza:
“Na kifungo chao kitajulikana baada ya tathmini ya baraza hilo la
maadili ambalo ikumbukwe kwamba kazi hiyo ya kutathmini haishi ndani ya
siku moja. Inaweza kuwa siku mbili, wiki moja, au miezi kwa sababu
kanuni haitubani. Na baada ya kumalizika itapelekwa kwenye Kamati Kuu
ambayo ndiyo itatoa maamuzi.”
Nape aliongeza kuwa tathmini ndiyo itaamua juu ya adhabu hizo
kulingana na utekelezaji wao katika adhabu walizokuwa wamepewa kama
wametekeleza ipasavyo au laa.
Makada hao walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na Kamati Kuu ya chama
hicho Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni
mapema za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati, kinyume cha
kanuni za uongozi na maadili za CCM, toleo la Februari 2010, Ibara
6(7)(i).
Ilielezwa wakati huo kuwa baada ya kuhojiwa, wote walithibitika
kufanya vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ndani ya chama hicho.
Adhabu hiyo, pamoja na mambo mengine, ililenga kuwachunguza makada hao pamoja na kutakiwa kujirekebisha.
Pia kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa kuwachunguza na kuchukua
hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine kufanyika kwa
vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.
Februari 13, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM chini ya Rais Jakaya
Kikwete ilifanya kikao chake Kisiwandui, Zanzibar na kuagiza adhabu kali
zichukuliwe dhidi ya wale watakaobainika kuwa walikiuka masharti ya
adhabu waliyopewa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula, ambaye kamati
anayoiongoza ndiyo iliyopewa kazi ya kufanya tathmini hiyo, alipotafutwa
na gazeti hili jana simu yake iliita mara mbili bila kupokewa na
alipopigiwa kwa mara ya tatu, simu yake hiyo ilidhihirika kuwa imezimwa.
KUELEKEA UCHAGUZI MKUU
Wakati CCM ikibaki kimya kueleza hatma ya makada wake sita na pia
kutangaza rasmi mchakato wa kuwapata wagombea wake wa nafasi mbalimbali
katika uchaguzi mkuu mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, tayari vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), kila kimoja kwa nyakati
tofauti kimeshatangaza ratiba na utaratibu wa makada wao kuchukua fomu
za kuwania nafasi mbalimbali.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza ratiba
na kueleza utaratibu wa kuchukua fomu za kuwania nafasi za ubunge,
uwakilishi na udiwani ambazo zitaanza kutolewa Mei 3 kwenye ofisi za
majimbo yote nchini.
Akitangaza utaratibu huo hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk.
Wilbrod Slaa, alisema fomu zitaanza kutolewa Mei 3, hadi Agosti 9 na
kwamba, uteuzi wa awali wa wagombea udiwani utafanywa na kamati tendaji
ya Kata kati ya Julai Mosi na wakati uteuzi wa wabunge na wawakilishi
utafanywa na kamati tendaji ya Jimbo kati ya Agosti 2 na 9 mwaka huu.
Tofauti na kipindi kilichopita, kazi ya uteuzi wa awali wa wagombea
ubunge kupitia viti maalumu itafanywa na Baraza la Wanawake la Chama
hicho(Bawacha), Agosti 8 mwaka huu na ambapo halmashauri kuu ya chama
hicho itathibitisha majina ya wagombea ubunge wote Agosti 10 mwaka huu.
Dk. Slaa alisema Baraza Kuu la chama ndilo litakalopendekeza jina la mgombea urais, mgombea mwenza na mgombea urais Zanzibar.
Alisema uteuzi wa mgombea urais pamoja na ilani ya chama hicho
vitathibitishwa Agosti 12 mwaka huu wakati ratiba ya kuchukua fomu na
kurejesha itatolewa na Kamati Kuu itakapokutana tena.
Kwa upande wake, Chama cha Wananchi (CUF) mwishoni mwa wiki
kilizindua mkakati maalum wa ushindi utakaotekelezwa na kamati za
uchaguzi, kuanzia ngazi ya tawi, hadi taifa.
Katika uzinduzi huo, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad,
alisema miaka yote ya uchaguzi mkuu wamekuwa wakijiandaa katika miezi
ya Juni na Julai, lakini mwaka huu wameamua kufanya maandalizi ya aina
yake mapema kwa kuwa wanaamini kuwa waklifanya hivyo watatimiza malengo
na kupata ushindi .
Alisema ili kufanikisha ushindi huo, kuanzia sasa kazi za ofisini
na za utawala wa chama chao hazina nafasi na kwamba, wajumbe wa kamati
tendaji za chama wamebadilika na kuwa wajumbe wa kamati za kushughulikia
uchaguzi.
Chama cha NCCR- Mageuzi kimetangaza rasmi kuanza kwa zoezi la
uchukuaji fomu kwa wanachama wake wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali
katika uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Mosena Nyambabe, alisema fomu hizo
zitaanza kutolewa Machi 15 hadi Aprili 30 kwa nafasi za udiwani, ubunge
na urais.
Nyambabe, alisema hatua hiyo haiendi kinyume cha misingi ya vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutokana na wagombea
watakaopatikana baada ya kupigiwa kura za maoni watakwenda kupambana na
wenzao wa vyama vingine kwa ajili ya kumpata mgombea mmoja. Alisema
utaratibu wa uchukuaji fomu kwa nafasi ya udiwani utaanza Machi 15 na
kumalizika Machi 30.
Alisema kwa upande wa ubunge na uwakilishi kwa Zanzibar, fomu
zitatolewa Machi 20 hadi 21. Kwa nafasi ya urais, fomu zitatolewa Aprili
Mosi hadi 30.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment