Kamanda wa Polisi wa Temeke, Kihenya Kihenya.
Katika tukio hilo lililotokea jana, majambazi wanne wakiwa na
silaha wakitumia pikipiki, walimpiga risasi ya mguuni dereva wa bodaboda
aliyekuwa katika harakati za kuziokoa fedha hizo na kusababisha kifo
chake wakati akikimbizwa hospitalini kutokana na kuvuja damu nyingi.
Tukio hilo la ujambazi lilitokea jana saa 2:30 usiku na kuendelea
kwa takriban nusu saa katika eneo la Vijibweni, karibu na mahali
linapojengwa daraja la Kigamboni, wilaya ya Temeke, jijini Dar es
Salaam.
Mmoja wa majambazi hao alikamatwa na wananchi na kushambuliwa hadi
kufa, huku wenzake watatu wakifanikiwa kutokomea kusiko julikana.
Hata hivyo, sanduku ambalo lilipatikana baada ya kuuawa kwa
jambazi huyo, lilikutwa likiwa na Sh. 700 na nyaraka za kikundi hicho na
baadhi ya raia katika eneo hilo waliwatuhumu polisi kwamba ndiyo
waliochukua fedha hizo kutokana na mazingira tata ya upotevu wa fedha
hizo.
Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa wanachama wa kikundi hicho
cha Vicoba chenye wanachama 30, Amanda Mushi, alisema hadi sasa
haijulikani aliyechukua fedha hizo kwani jambazi aliyekuwa na sanduku
hilo aliuawa na wananchi baada ya kukimbilia kwenye makazi ya watu na
wenzake watatu kutokomea kusikojulikana.
Kwa mujibu wa Amanda, waendesha bodaboda na majambazi hao
walifukuzana kwa dakika kati ya tano au 10 kabla ya kukamatwa mmoja wao
aliyekuwa na mkoba huo na kuuawa na wananchi wenye hasira.
“Sanduku limepatikana, halina kitu…limekutwa na Sh. 200 na noti ya
Sh. 500 maeneo ya Kigamboni katika kituo cha mafuta mwendo wa dakika
tano au kumi kwa pikipiki kutoka eneo la tukio,” alisema Amanda na
kuongeza:
“Askari alisema walipofika eneo la tukio walilikuta mkoba huo ukiwa
linazagaazagaa eneo hilo…wakaamua kulichukua na walipoangalia ndani
walikuta halina kitu isipokuwa kiasi hicho cha fedha na nakala.”
Alisema viongozi wa kikundi hicho akiwamo mwenyekiti, katibu na
mhazini wametakiwa kuripoti kituo cha polisi kutoa maelezo juu ya tukio
hilo la uporaji.
Kwa mujibu wa taarifa nyingine ambazo NIPASHE lilizipata,
mwenyekiti huo wa kikundi hakupatwa na madhara yoyote zaidi ya
kunyang’anywa simu yake wakati majambazi hao walipofika nyumbani kwake
na kuingia ndani na kumtaka kutoa fedha na alipogoma walichukua fedha
hizo kwa nguvu na kutokomea nazo.
Inadaiwa kuwa, mume wa mwenyekiti a huyo hakuwapo wakati tukio hilo linatokea.
Hata hivyo mwenyekiti huyo alipoulizwa, alisema mume wake alikuwa
safarini Morogoro, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa, mume wake
alipotafutwa na kuulizwa alijibu hakuwapo eneo la tukio hivyo hajui
chochote kilichotokea.
Juhudi za kumtafuta mwenyekiti huyo ili aweze kuzungumzia tukio
zima lilivyokuwa, hazikuzaa matunda baada ya kupewa taarifa kwamba kwa
wakati huo hakuwa na mawasiliano na kwamba alikuwa mbali.
Kwa mujibu wa taarifa zilizolifikia gazeti hili kupitia vyanzo
tofauti, polisi walionyeshwa sanduku hilo na kwamba aliyelikamata na
kulipeleka kituoni alilikuta limeshavunjwa na fedha kuchukuliwa.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Temeke,
Kihenya Kihenya, alisema mbali na mauaji hayo, jumla ya Sh. milioni nane
ziliporwa na kwamba haijulikani aliyetokomea na fedha hizo.
Akifafanua, RPC Kihenya, alisema majambazi hao wakiwa wanne,
walifika nyumbani kwa mwenyekiti wa kikundi hicho katika eneo hilo,
kimya kimya na kumtaka awape fedha walizodai amepewa ili kuzihifadhi.
Kwa mujibu wa RPC Kihenya, mwenyekiti huyo alikataa kwa kuwaambia
hana fedha huku akipiga kelele kuomba msaada kwa majirani wakiwamo
madereva wa bodaboda waliokuwa karibu na eneo hilo.
“Kimsingi kuna tukio limetokea la watu kujaribu kupora Sh. milioni
nane mali ya kikundi cha kinamama wa Vicoba eneo la Vijibweni,” alisema
kamanda huyo na kuongeza:
“Mama mmoja ambaye ni mwenyekiti wao, ndiye anayetunza fedha. Wale
jamaa waliingia kimyakimya na kumtaka azitoe hizo pesa. Alipiga kelele
kutaka msaada kwa madereva wa bodaboda ambao walifika hapo na
kumsaidia,” Alisema na kuongeza:
“Wale majambazi wakazichukua zile fedha kimyakimya bila kutumia
bunduki na kuanza kukimbia nazo, huku wakifukuzwa na waendesha
bodaboda.”
Alisema wakiwa katika purukushani hiyo ya kukimbizana, dereva wa
bodaboda na wenzake wawili, walikuwa wakipiga kelele katika barabara
waliyokuwa wakifukuzana.
“Baada ya kuona wamelemewa, mmoja wa majambazi hao wanne aliyekuwa
amekaa katikati, akachomoa bunduki na kumpiga risasi mguuni dereva wa
bodaboda hiyo na kumwacha akianguka na kuvuja damu nyingi.”
“Kelele hizo ziliwaamsha watu wengi na kuanza kuwaandama wahalifu
hao ambao baada ya kuzidiwa nguvu, waliamua kukimbia hovyo kwenye makazi
ya watu.”
Alisema wananchi wenye hasira walifanikiwa kumkamata na kumuua
jambazi mmoja, ambaye alikuwa amebeba sanduku lililokuwa na kiasi hicho
cha pesa, huku watatu wakifanikiwa kukimbia.
Kwa mujibu wa kamanda huyo, baada ya polisi kuwasili katika eneo la
tukio, walikuta jambazi huyo ameshafariki na sanduku hilo la fedha
lilikutwa likiwa halina kitu mbali na eneo la tukio na kwamba
haijulikani aliyezichukua fedha hizo.
Alisema dereva huyo wa bodaboda alifariki dunia njiani akikimbizwa
hospitali kutokana na kuvuja damu nyingi na kuwaacha wenzake wawili
wakiwa wamejeruhiwa.
Mwili wa dereva huyo umehifadhiwa katika hospitali iliyopo katika
eneo hilo la Vijibweni, huku wa jambazi ukitarajiwa kuhamishwa kutoka
hapo kwenda hospitali ya Temeke kwa uchunguzi zaidi.
Alisema kwa sasa polisi wanaendelea na upelelezi dhidi ya majambazi waliohusika na tukio hilo kwa ujumla.
Kamanda huyo aliwashauri wananchi kuwa na utamaduni wa kuhifadhi
fedha zao benki wanapokuwa na kiasi kikubwa cha fedha na pia kuomba
msaada wa vyombo vya usalama wanapozipeleka au kuzichukua benki.
CHANZO:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment