Home » » UTEKELEZAJI MKATABA WA KYOTO UMEKWAMA - MTAALAMU

UTEKELEZAJI MKATABA WA KYOTO UMEKWAMA - MTAALAMU

 
Rais Jakaya Kikwete.
Utekelezaji  wa mkataba wa Kyoto wa kupunguza hewa ukaa kwa nchi zenye viwanda vingi duniani, umeshindwa kutekelezwa hali ambayo imechangia ongezeko la joto duniani.
 
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira, Francois Gemenne, aliyasema hayo wakati wa mjadala wa hatua za kuchukua katika kukabiliana na mabadiliko hayo kwa Tanzania na mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa.
 
Mjadala huo uliandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa na kufanyika katika Kituo cha utamaduni cha Ufaransa na kuhudhuriwa na  wadau mbalimbali na wazungumzaji walikuwa ni Mkurugenzi wa kituo cha mafunzo ya mabadiliko ya tabia nchi (CCCS) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Pus Yanda, Mratibu wa Forum CC, Rebecca Muna na mtaalamu wa mabadiliko ya tabia nchi wa Shirika la kimataifa la Uhamiaji (IOM), Alex Flavell.
 
Alisema nchi za China, Brazil, India, Mexco na Russia, zilitajwa kuwa zinaongoza kwa kuzalisha hewa ukaa na kutakiwa kupunguza kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2013, lakini hadi sasa hakuna hatua zilizochukuliwa na hivyo kumekuwepo na ongezeko kubwa kwa viwanda vinavyozalisha hewa ya ukaa.
 
Naye Mratibu wa Forum CC, Rebecca Muna, akizungumzia jinsi jamii ya Tanzania ilivyoathirika na mabadiliko ya tabia nchi, alisema ni kuwepo kwa mabadiliko ya vipindi vya mvua, ongezeko la joto, magonjwa mapya yanayoshambulia mimea, mbegu hazioti, mafuriko na ukame wa muda mrefu.
 
“Utafiti wetu ulibaini kuwa wengi hawana uelewa, lakini viashiria vya athari za mabadiliko ya tabia nchi ni vya wazi, ukitembelea ukanda wa Pwani watakueleza kwa sasa wanafuatilia samaki kwenye eneo lenye kina kirefu tofauti na zamani, na baadhi ya visiwa kumezwa,” alisema.
 
Naye, Prof. Yanda, alipoulizwa iwapo ujio wa gesi asilia utasaidia kupunguza mabadiliko ya tabia nchi, alisema tatizo kubwa ni miundombinu ya miji na majiji ya Tanzania ambayo itakuwa vigumu kufikisha nishati ya gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani.
 
Naye, Flavell alisema uhamaji wa watu kutoka eneo moja kwenda jingine kinachangia uharibifu wa mazingira na hivyo kuwa sababu ya mabadiliko ya tabia nchi na kwamba maeneo ya mijini kumpa ongezeko kubwa la watu ambao kwa namna moja hawasaidii waliobaki vijijini kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
 
Alisema kwa asilimia kubwa mabadiliko hayo yanasababishwa na binadamu ambaye anategemea kuendesha maisha yake katika eneo la dunia, kwa shughuli za kusafisha mashamba kwa ajili ya kilimo, ujenzi wa miundombinu, uchomaji mkaa na shughuli nyingine.
 
Hivi karibuni, Rais Jakaya Kikwete, alizokutana na Rais wa  Ujerumani, alimweleza kuwa ujio wa gesi ni tumaini jipya kwa wakazi wa Dar es Salaam, ambao hutegemea nishati ya mkaa kwa tani 40 kwa mwaka, jambo ambalo limechangia uharibifu wa mazingira kwa kiasi kikubwa.
 
Ufaransa inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi duniani, utakao fanyikia Paris.
 
SOURCE: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa