Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili (MNH), inatarajia kuanzisha kitengo cha magari ya
kubebea wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya kubeba wagonjwa kutoka katika
maeneo mbalimbali ya Jiji.
Hayo yalielezwa jana na Mkurugenzi wa MNH, Dk. Hussein Kidanto,
wakati wakisaini makubaliano ya kupokea msaada wa magari mawili ya
kubebea wagonjwa kutoka kwa Balozi wa Japan nchini, Masaki Okada.
Pia, Balozi Okada, alitoa msaada wa mashine ya kukamulia mafuta ya Alizeti katika wilaya ya Chato mkoani Geita.
Dk. Kidanto, alisema kwa sasa hospitali hiyo ina gari moja la
wagonjwa ambalo linashindwa kukusanya wagonjwa na kuwapeleka katika
hospitali hiyo na chini ya kitengo hicho wataanza na magari 10.
“Tunaushukuru Ubalozi wa Japan kwa kutoa msaada huu, utakuwa mwanzo
wa kuanzisha kitengo cha huduma ya magari ya wagonjwa ambacho
tunakianzisha Muhimbili ili yaweze kuwabeba kutoka maeneo mbalimbali ya
Jiji,” alisema Dk. Kidanto.
Alifafanua kuwa, magari hayo yataandikwa namba maalum za maeneo
tofauti ya Jiji na yatabeba watu watakaopatwa na ugonjwa wa ghafla kama
mama wajawazito, wenye magonjwa ya moyo na maengine kwa lengo la
kuwafikisha hospitali wakiwa salama.
Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ambaye pia ni
Mbunge wa Chato, alimshukuru Balozi hiyo kwa kusaidia kutoa msaada huo
wa magari ya wagonjwa pamoja na mashine ambayo aliiahidi kuitoa
alipotembelea wilaya hiyo.
SOURCE:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment