Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, amesema kila Kata nchini,
itapata nakala 300 za Katiba inayopendekezwa na kwamba tayari serikali
imeshaanza kuisambaza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema kuna zaidi kata
3,800 nchini kote na lengo la Serikali kuhakikisha inasambaza nakala
hizo kwenye vijiji, vitongoji na mitaa kupitia Ofisi za Wakuu wa Mikoa,
wilaya na wakurugenzi wa Halmashauri za miji, manispaa na majiji.
Alisema tayari serikali imeanza kusambaza nakala milioni mbili za
Katiba inayopendekezwa nchini kote ili kuwawezesha wananchi kuisoma na
kushiriki katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka
huu.
Alisema kati ya nakala hizo, nakala 1,800,000 zinasambazwa Tanzania Bara na nakala 200,000 zinasambazwa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Waziri Migiro, hadi kufikia jana, jumla ya nakala
707,140 zilikuwa zimesambazwa katika mikoa 12 ya Tanzania Bara na
Zanzibar ambayo imepata nakala 200,000 na kuwa kazi hiyo inaendelea
vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda mfupi ujao.
Mikoa hiyo na nakala ziliozosambazwa katika mabano ni Katavi
(15,640), Rukwa (27,040), Ruvuma (47,740), Mbeya (78,640), Simiyu
(34,840), Mara (52,540), Tabora (58,540) na Kigoma (41,440). Mikoa
mingine ni Kagera (54,340), Geita (36,940), Mwanza (57,040) na Pwani
ambapo usambazaji umeanza kwa wilaya ya Mafia ambayo imepata nakala
2,400.
“Idadi ya nakala ya Katiba inayopendekezwa kwa kila mkoa inategemea
na wingi wa kata katika mkoa, ndiyo maana baadhi ya mikoa unaona
imepata nakala nyingi,” alisema Dk. Migiro.
Aidha, alisema Serikali imepanga kusambaza nakala 658,400 kwa
taasisi za elimu, dini, vyama vya siasa na asasi za kiraia na kuwa
usambazaji huo utaanza hivi karibuni.
Hata hivyo, mchanganuo wa mikoa inayotajwa kupata nakala hiyo kwa
Tanzania Bara na Zanzibar, unaonyesha kuwa nakala zilizosambazwa ni
741,300 na siyo milioni mbili kama Waziri alivyoeleza na hata hesabu za
kila kata kupata nakala 300 kwa kata 3,800 ni nakala 1,140,000.
SOURCE:
NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment