Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akitoa
ufafanuzi wa mfumo wa kielektroniki utakaosimamia utoaji wa huduma
katika sekta ya ardhi.
……………………………………………………………………………
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Dar es salaam.
SERIKALI imeanza kutekeleza
mpango wa kusimika mfumo funganishi wa kielektroniki (Intergrated Land
Management Information Systeam) utakaosimamia sekta ya ardhi nchini na
kupunguza muda, gharama za upimaji na upatikanaji wa hati miliki za
ardhi kwa wananchi.
Akizungumzia uanzishwaji wa
mfumo huo leo jijini Dar es salaam, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema mfumo huo wa kisasa utawawezesha
wananchi kupata hati za umiliki wa ardhi na taarifa zao za malipo na
matumizi ya ardhi katika ngazi za vijiji, wilaya, kanda hadi taifa.
Amesema utekelezaji wa mradi
huo utasimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa
ufadhili wa Benki ya dunia kupitia ofisi ya Waziri Mkuu na kuongeza kuwa
utekelezaji wa mradi huo utafanyika kwa awamu mbili itakayohusisha
uundwaji wa programu hiyo na majaribio ya mfumo huo katika kanda
zilizochaguliwa za mikoa ya Dar es salaam,Pwani na Morogoro.
Mhe. Lukuvi ameeleza kuwa
utekelezaji wa mradi huo mkubwa pia utaambatana na utoaji wa hati mpya
za umiliki wa ardhi na kufuta za zamani, upigaji wa picha za anga kwa
mfumo wa Satelite, ujenzi wa kituo cha kutunza kumbukumbu za ardhi
kitaifa pamoja na uelimishaji wa jamii kuhusu matumizi ya mfumo huo.
Amesema awamu kwanza
itatekelezwa kwa muda wa miaka miwili kuanzia Machi 2015 hadi 2016 na
kugharimu kiasi cha dola za Kimarekani milioni 35 huku awamu ya pili
ikihusisha uboreshaji wa mfumo huo kutokana na matokeo mazuri
yatakayopatikana kwenye awamu ya kwanza ili kuwezesha mfumo huo
kusambazwa nchi nzima.
Akitaja faida za kusimikwa kwa
mtambo huo nchini amesema utasaidia kuhifadhi taarifa za wananchi kwa
uhakika na usahihi pamoja na matumizi ya ardhi kote nchini pia
utarahisisha upatikanaji wa hati za umiliki wa ardhi kwa wananchi wengi
zaidi tofauti na ilivyo sasa kutokana na ongezeko la kasi ya upimaji wa
ardhi
Aidha, amesema mfumo huo
utaondoa vitendo vya utoaji wa hati zaidi ya moja kwenye viwanja,
kuondoa hati pandikizi na kuongeza uwazi wa taarifa kwa kuwawezesha
wananchi wanaomiliki ardhi kupata taarifa zao kupitia simu za mkononi.
“Nawahakikishia watanzania kiama
cha matapeli wa ardhi kimefika ,teknolojia hii ni ya kisasa na Tanzania
itakua nchi ya pili barani Afrika kuwa na mfumo wa aina hii, Serikali
tumelenga kuondoa kabisa kero na ukiukaji wa maadili uliokuwa ukifanywa
na baadhi ya watendaji wa serikali wasio waaminifu katika utoaji wa
hati za viwanja nchini” Amesisitiza.
Amefafanua kuwa kufungwa kwa
mitambo hiyo ya kielektroniki katika kanda 7 nchini kutawezesha kila
sehemu ya ardhi kupimwa na kuongeza thamani ya ardhi na mapato ya
Serikali yatokanayo na ardhi huku na kueleza kuwa nchi ya Uganda ambayo
sasa inatumia mfumo huo imenufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwa na
taarifa sahihi za ardhi na matumizi yake.
Amewataka wananchi na watendaji
wanaosimamia sekta ya ardhi kote nchini wajiandae kupokea mabadiliko
hayo kwa kuanza kutunza kumbukumbu sahihi za za viwanja wanavyomiliki
ambazo zitaingizwa kwenye mfumo huo na wao kupewa hati mpya za
kielektroniki.
Pia amewatoa hofu wananchi kuwa
zoezi la upimaji wa maeneo ambayo bado hajapimwa hususani yale yenye
hati zilizotolewa na vijiji na zile za kimila katika maeneo mbalimbali
nchini litaenda sambamba na utoaji wa hati mpya za kielektroniki.
Katika hatua nyingine Mhe.
Lukuvi amesisitiza kuwa zoezi la bomoa bomoa linalosimamiwa na wizara
yake katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam sasa litafanywa
katika mikoa mingine kwa lengo la kusimamia sheria ya ardhi namba 4 ya
mwaka 1999 kifungu namba 175(1) inayozuia mwananchi yeyote kuingia na
kuendeleza kwenye ardhi asiyoimiliki kisheria.
“Naomba wananchi watupe
ushirikiano,haki lazima itendeke kazi hii tumeianza katika jiji la Dar
es salaam na tunaendelea nayo katika maeneo mengine nchini ambako kuna
vitendo vya dhuruma na uvamizi wa ardhi unaofanya na baadhi ya watu
kinyume cha sheria”
0 comments:
Post a Comment