Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda pamoja na wajumbe wa kamati ya uongozi ya Bunge wakitembelea mradi wa daraja la kisasa linalojengwa na NSSF kwa ubia na Serikali kuunganisha Jiji la Dar es Salaam na mji wa Kigamboni.
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SPIKA wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda amelipongeza Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa miradi mikubwa mbalimbali linayoendelea kuwekeza nchini ambayo imekuwa chachu ya maendeleo na kukuza hadhi ya nchini.
Spika Makinda ametoa kauli hiyo jana alipokuwa akitembelea baadhi ya miradi mikubwa ya NSSF iliyopo jijini Dar es Salaam, ukiwemo mradi wa ujenzi wa daraja la kubwa la kisasa linalojengwa kuunganisha Jiji la Dar es Salaam na Mji wa Kigamboni pamoja na mradi mkubwa wa ujenzi wa Mji wa Kisasa unaojulikana kwa jina la Dege ECO Village unaojengwa kwa ubia pamoja na ujenzi wa nyumba za kisasa zenye hadhi mbalimbali kulingana na mahitaji ya watu.
Akizungumza wakati akitembelea miradi hiyo, Makinda alisema miradi hiyo mbali na kuleta maendeleo nchini inakuza hadhi ya nchi pamoja na kuirahisishia serikali katika utoaji huduma kwa wananchi wake.
Aliiomba Serikali kupitia Wizara mbalimbali na jamii nzima kuendelea kutoa ushirikiano dhidi ya miradi hiyo kwani inachangia maendeleo kuanzia ngazi ya jamii pamoja na taifa kwa ujumla. Aliwataka wananchi kutumia fursa iliyopo ya kununua na kukopa nyumba zinazojengwa na shirika hilo kwani mbali na kujengwa kwa hadhi anuai na kisasa zimepangiliwa jambo ambalo linarahisisha utoaji wa huduma za jamii dhidi yao.
Alisema kwa maendeleo ya sasa ni nchi ya Tanzania pekee ambapo raia wake hujenga nyumba wenyewe, kwani mataifa mengi yaliyoendelea nyumba hujengwa na mashirika na kuuzwa kwa raia jambo ambalo huchangia kwa kiasi kikubwa uwepo wa miji iliyopangiliwa tofauti na ilivyo Tanzania.
“…Duniani kote watu wanaojenga nyumba wenyewe hadi sasa ni Tanzania tu, na hii ndio chanzo kikubwa cha nchi yetu kuendelea na kuwa na miji ambayo haijapangiliwa (ujenzi holela). Lazima tubadilike unajua ukiwa na mji uliopangiliwa ni rahisi hata kuwahudumia wananchi wako…,” alisema Makinda.
Aidha alishauri uwepo wa utaratibu mzuri wa kukopesha nyumba za kisasa zinazojengwa na NSSF ili wahitaji wapewe na kulipa kwa awamu huku wakimilikishwa nyumba hizo jambo ambalo litaondoa adha ya upatikanaji wa makazi bora kwa wananchi.
Katika ziara hiyo Spika Makinda aliambatana na Waziri wa Fedha Saada Mkuya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama , Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka pamoja na Kamati ya Uongozi ya Bunge la Tanzania ambao kwa pamoja walilipongeza Shirika la NSSF na kushauri kuendelea kuwekeza pia katika mikoa mingine inayochipukia kimaendeleo kwa sasa ili kusambaza huduma maendeleo mengine.
Awali akitoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa daraja la kisasa la Kigamboni, Meneja Mradi wa NSSF, Mhandisi John Msemwa alisema licha ya changamoto zilizojitokeza mradi huo hadi sasa umekamilika kwa asilimia 75 ya ujenzi wake.
Kwa upande wake, Mhandisi Juhus Nyamuhokya wa kampuni ya Ujenzi ya Hifadhi wabia wa NSSF katika ujenzi wa Kijiji cha kisasa cha ‘Dege ECO Village’ kinachojumuisha ujenzi wa nyumba 7,460 za kisasa zenye hadhi tofauti kulingana na mahitaji alisema ujenzi wake utajumuisha miaka minne ukijengwa kwa awamu tatu.
Mhandisi Nyamuhokya alisema awamu ya kwanza ya mradi huo inakamilika Desemba 2015, awamu ya pili itakamilika Desemba 2016 huku awamu nyingine ikitarajiwa kukamilika Desemba 2017.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Ramadhani Dau alimshukuru Spika wa Bunge la Tanzania Anne Makinda pamoja na wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Bunge kwa kutembelea miradi hiyo ambayo ina lengo lakuchochea maendeleo ya taifa na wananchi kiujumla.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment