Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Naibu
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, John
Mnyika, amesema kauli ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka wahisani
waiheshimu serikali na kwamba wasitoe misaada kwa masharti, imetokana na
hasira za rais baada ya kuanikwa na magazeti ya Marekani juu ya sheria
zinazodaiwa kutungwa kwa ajili ya kuminya uhuru wa habari na utoaji wa
taarifa.
Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, alisema kitendo cha
wahisani kugomea kuchangia msaada wao katika mfuko wa bajeti
kimesababishwa na kukithiri kwa ufisadi hasa katika sekta za maji, afya
na kashfa ya Escrow.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mnyika alisema ufisadi
uliofanyika kuanzia ngazi ya wizarani hadi kwenye halmashauri ambao
umekwamisha miradi ya maendeleo maeneo mbali mbali nchini, umesababisha
wahisani kuiwekea ‘mguu chini’ serikali ambayo badala ya kuchukua hatua,
inaanza kugombana na nchi wahisani suala ambalo amedai kuwa litaiwekea
mazingira magumu serikali ijayo.
“Kama Rais Kikwete angekuwa na dhamira ya dhati ya serikali yake
kuwa na sauti anayotaka kutuaminisha sasa ili iheshimiwe, isichezewe,
angeonesha kupitia bajeti hii ya sasa. Huwezi kusema kuwa nchi inaweza
kwenda bila misaada ya wahisani wakati huo huo utekelezaji wa bajeti
yake ya mwaka 2015/16 inayojadiliwa sasa bungeni bado inategemea
wahisani hao hao wasaidie.
“Kama Rais Kikwete angetaka kudhihirisha kuwa serikali yake ni
imara na inaweza kuifanya nchi ijitegemee bila kusubiri misaada ya
wahisani angesema maneno haya na kufanya kwa vitendo kuanzia mwaka 2005
alipoingia madarakani au 2010 alipoingia madarakani kwa mara ya pili,
vinginevyo kuisema sasa hivi wakati amebakiza miezi michache kuondoka
madarakani ni kutaka kuitengenezea mazingira mabaya serikali ijayo
ambayo haitakuwa ya CCM," alisema na kuongeza:
“Sasa baada ya ufisadi kuzidi kwenye serikali yake, huku kukiwa na
udhaifu mkubwa wa uwajibikaji na hatua hazichukuliwi, wahisani wameamua
kuweka msimamo hivyo imepelekea miradi mingi ya maendeleo kukwama,
badala ya serikali kuchukua hatua, rais anawatishia wahisani, hizi ni
hasira za Rais baada ya magazeti ya Marekani kumwanika kuwa serikali
inatunga sheria mbaya za kuminya uhuru wa habari na utoaji taarifa."
“Kwa sababu CCM haiwezi kusaidia nchi hii kujitegemea suluhisho
hapa ni kukiondoa madarakani chama hiki kwanza. Watanzania wajiandae
kuiweka Serikali ya Ukawa ili ishughulikie na kuondoa ufisadi, ipanue
wigo wa vyanzo vya ndani katika kuongeza mapato na kudhibiti matumizi
makubwa ya anasa na kubadili mfumo wa utawala,” alisema Mnyika.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment