Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imeibuka mshindi wa tuzo ya mdhibiti bora wa nishati barani Afrika kwa mwaka 2015 huku ikieleza kuwa hatua hiyo itawavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
Akizungumza juzi Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi alisema tuzo hiyo inalenga kuwatambua wadhibiti wa nishati na maji waliotoa mchango mkubwa katika Afrika.
Alisema baada ya nchi mbalimbali za Afrika kuchujwa, nchi tano zilichaguliwa ili kushindana ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Mali na Cameroon.
Alisema taasisi zilizoshindanishwa ni Mamlaka ya Udhibiti wa Umeme ya Camoroon (ARSEL), Kamisheni ya Udhibiti wa Umeme na Maji ya Mali (CREE), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Uganda (Era) na Kamisheni ya Udhibiti wa Nishati ya Kenya na Ewura.
Alisema Tanzania ilishinda tuzo hiyo kwenye Jukwaa la Nishati Afrika (AEF) lililofanyika Juni 8 hadi 11 mwaka huu, Dubai, Uarabuni na limekuwa likifanyika kila mwaka kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa nishati.
Alisema mshindi wa tuzo hiyo alichaguliwa na kamati yenye kujumuisha jopo la wataalamu wa Shirika la EnergyNet la Uingereza.
Ngamlagosi alisema tuzo hiyo inaifanya Tanzania kutambulika kimataifa kama nchi yenye taasisi makini ya udhibiti wa sekta ya nishati na maji.
“Kwa nafasi hiyo, Tanzania sasa itashuhudia upatikanaji wa kiwango cha juu wa mitaji ya uwekezaji wa kutoka nje kwenye sekta ya nishati na maji,” alisema.
Ngamlagosi alisema mafanikio hayo yalitokana na Ewura kuweka wazi kanuni za uzalishaji, usambazaji na uuzaji wa umeme.
“Tumeweka pia mikataba elekezi ya namna ya kuuziana umeme, mikataba hii inapokuwa wazi inawafanya wawekezaji kuchagua nchi yetu kuja kuwekeza,” alisema.
Akizungumzia mkutano huo, Ngamlagosi alisema mbali na kuhudhuriwa na watendaji wa Serikali za Afrika, pia huhudhuriwa na wawekezaji wa kimataifa wenye kiu ya kuwekeza kwenye umeme.
“Tuzo inaifanya Tanzania sasa kutambulika kama nchi yenye taasisi thabiti ya udhibiti wa sekta ya nishati na maji. Ushindi huu utaleta imani kwa wawekezaji katika kuvutia mitaji binafsi kwenye sekta ya nishati,” alisema Ngalamgosi.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment