Home » » MALINZI AKOMAA NA NOOIJ WAKE

MALINZI AKOMAA NA NOOIJ WAKE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.
Licha ya kelele za wadau wengi wa soka kutaka kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij atimuliwe, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amemkingia kifua.
Baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Misri mwishoni mwa wiki katika mchezo wa kwanza wa kusaka tiketi ya fainali za mataifa ya Afrika (Afcon 2017), wadau wa soka wamekuwa wakishinikiza Nooij atimuliwe.
Malinzi aliliambia gazeti hili jana kuwa TFF haitomfukuza kocha huyo hadi timu hiyo itakaposhindwa kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan).
“Kuhusu hatima ya kocha, kamati ya utendaji ilishatoa msimamo wake kuwa anatakiwa kuhakikisha timu inafuzu Chan. Iwapo akishindwa kufanya hivyo, hakuna namna tutaachana naye,” alisema Malinzi.
Stars itaanza kampeni yake ya kusaka tiketi ya Chan 2016 mwishoni mwa wiki kwa kuivaa Uganda kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar na kurudiana wiki mbili baadaye jijini Kampala, Uganda.
Wakati huohuo, TFF limeingia mkataba na Kampuni ya GS1 kwa ajili ya kudhibiti utengenezaji na mauzo holela ya jezi za Taifa Stars.
Kulingana na mkataba huo, kuanzia sasa jezi za Stars zitakuwa na nembo maalumu ambayo itatumika kutofautisha jezi halisi na zile bandia ambazo zimekuwa zikitengenezwa na kuuzwa kwa wingi nchini.
Malinzi alisema jana kuwa kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua mojawapo ya shirikisho hilo kutafuta mwarobaini wa kutibu tatizo sugu la biashara holela ya jezi bandia.
Mkurugenzi Mtendaji wa GS1, Fatma Kange alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huo kutalisaidia shirikisho hilo kujiongezea mapato yake na pia kuleta hamasa na uzalendo kwa timu ya Taifa.
“Mtu anapovaa jezi halisi anakuwa na ari ya kupenda na kujisikia fahari kuchangia soka,” alisema.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa