Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Umoja wa watendaji wakuu wa kampuni wa CEO RoundTable (CEOrt) umeandaa mdahalo wa kuzungumzia mbio za urais utakaowahusisha viongozi wa vyama vya upinzani, Profesa Ibrahim Lipumba, Dk Willibrod Slaa, Zitto Kabwe na Emmanuel Makaidi, lakini Chadema imesema itakuwa tayari kwa midahalo baada ya mchakato wa ndani kukamilika.
Kauli hiyo ya Chadema inaweza kuwa kikwazo kingine kwa CEOrt kuendesha midahalo hiyo baada ya wa kwanza uliokuwa uhusishe makada 10 wa CCM wanaoomba ridhaa ya chama hicho kuwania urais, kushindwa kufanyika kutokana na viongozi wa sekretarieti kutoa kauli tofauti siku moja kabla.
Kiongozi wa CEO, Ali Mufuruki alisema jana kuwa Dk Slaa, Profesa Lipumba, Makaidi na Zitto, ambaye ni kiongozi mkuu wa ACT-Wazalendo, wamethibitisha kushiriki kwenye mdahalo huo utakaofanyika kesho kuanzia saa 1:00 jioni jijini Dar es Salaam.
Lakini Dk Slaa aliiambia Mwananchi jana kuwa Chadema itakuwa tayari kushiriki kwenye midahalo baada ya kumaliza mchakato wa kupata mgombea wake na kukamilisha Ilani ya Uchaguzi, mambo ambayo alisema hupitishwa na vikao vya juu.
“Kamanda, sijui kama ni kongamano au mdahalo: 1. Chadema inaendeshwa kwa katiba, kanuni na taratibu zake. Hadi siku ya leo taratibu zetu hazijafikia kupata aspirants (watangazania),” alisema katibu huyo mkuu wa Chadema katika ujumbe wake mfupi wa simu.
“2. Kama kuna waliopata aspirants, Chadema bado mchakato wetu unaendelea. 3. Midahalo inafanywa kwa msingi wa ilani. Chadema ilani yetu haijafika bado mbele ya vikao vya maamuzi, yaani Baraza Kuu na Mkutano Mkuu. Hivyo tukienda mdahalo tutakuwa tunazungumzia ilani ipi?
“Hivyo tuko tayari kwa midahalo yote baada ya mchakato wetu wa ndani kukamilika.”
Mufuruku alikuwa ametuma taarifa hiyo kwenye ukurasa wake wa facebook na alipopigiwa simu na Mwananchi, alithibitisha kuwapo kwa mdahalo huo ambao alisema utaonyeshwa moja kwa moja na vituo vya televisheni, redio na intaneti.
Kuhusu ushiriki wa Zitto, ambaye atagombea ubunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mufuruki alisema CEOrt imemualika kwa kuwa ni kiongozi wa chama ambacho kinaweza kusimamisha mgombea wa urais.
“Kushiriki si lazima uwe unachukua fomu za kugombea urais. Yeye ni kiongozi wa chama ana mawazo yanayoweza kutoa mchango kwenye mdahalo,” alisema Mufuruki.
CEOrt imepanga kufanya midahalo kadhaa mwezi huu na Juni 25 itaendesha mdahalo utakaoshirikisha wagombea kutoka CCM baada ya kada mmoja tu, Balozi Amina Salum Ali, kujitokeza kwenye mdahalo wa kwanza na hivyo kusababisha uahirishwe.
Profesa Lipumba, ambaye amechukua fomu za kuomba ridhaa ya CUF kupitishwa kugombea urais kwa mara ya tano iwapo jina lake litapitishwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), aliiambia Mwananchi jana kuwa atashiriki kwenye mdahalo huo, kama ilivyo kwa Makaidi ambaye amepitishwa na NLD kuwania nafasi hiyo
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment