Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Tabia ya wanafunzi wa elimu ya juu kugoma ili kushinikiza
Serikali au uongozi wa chuo husika kufanya jambo fulani imeanza
kuzoeleka nchini.
Migomo hiyo huambatana na vurugu zinazosababishwa
aidha na wanafunzi kuamua kufanya fujo au askari polisi wakati
wakiwatawanya wanafunzi waliogoma.
Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala (Kiu)
kilichopo Dar es Salaam ni taasisi ya elimu ya juu ambacho hakiwezi
kuwekwa kando kati ya vyuo vinavyokumbwa na migogoro.
Chuo hicho kimetawaliwa na migomo ya wanafunzi wake kutokana na changamoto mbalimbali zinazoibuliwa na wanafunzi wake.
Vuguvugu la mgomo katika chuo hicho lilianza
Januari, 2011 baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba kilikuwa hakijasajiliwa
nchini, bali kilikuwa kikiendesha shughuli zake kinyume na sheria
inayotaka taasisi yoyote ya elimu ya juu kusajiliwa.
Wanafunzi walilalamika kukosa mikopo inayotolewa
na Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kwa sababu HESLB
haikukitambua chuo hicho.
Tatizo hilo liliendelea, licha ya uongozi wa chuo hicho kuwaambia wanafunzi kwamba kilikuwa kimesajiliwa.
Baadaye uliibuka mzozo mwingine juu ya ulipaji wa
ada. Wanafunzi walikuwa wakilipa ada zao kwa Dola ya Marekani. Walikataa
kuendelea kulipa kwa fedha hiyo baada ya kubaini kwamba wanalipa zaidi,
ikilinganishwa na vyuo vingine.
Serikali ilitoa agizo kwa chuo hicho kusitisha
ulipaji wa ada kwa Dola kwa wanafunzi wa Kitanzania. Hata hivyo
wanafunzi kutoka nchi nyingine wanaendelea kulipa kwa Dola.
Matatizo mengine
Wanafunzi wa Kiu wamebainisha matatizo
yanayokikabili chuo hicho. Baadhi ya matatizo hayo ni ufundishaji wa
Kozi ya Multi-Purpose Program(MPP), ambayo hutolewa kwa wanafunzi kabla
(MPP) hawajaanza rasmi kusoma shahada zao.
Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Shahada ya Famasia,
Ally Mustapha Said anasema kuwa wanapewa masomo mengi ya kusoma tena
kwa ada kubwa na muda mrefu kuliko inavyotakiwa.
Saidi anataja masomo 10 wanayofundishwa kuwa ni Kiingereza,
kompyuta, elimu ya viumbe (biolojia), kemia, hesabu, fizikia, maadili,
sayansi ya tabia (behavioral science), stadi za mawasiliano na
ujasiriamali.
“Jambo la kushangaza, masomo yote haya
tunafundishwa kwa muhula mzima, badala ya siku 72. Pia, tunaambiwa
tulipie ada kama tunayolipa kwenye masomo ya shahada. Serikali haijasema
chochote mpaka sasa, tunaendelea kulipa fedha nyingi,” analalamika
Said.
“Mwanafunzi huyo anasema kuwa ikiwa mtu amefeli
masomo ya msingi (elimu ya viumbe, kemia na fizikia), atalazimika
kurudia kozi nzima ya MPP, badala ya masomo aliyofeli,” anasema
akiongeza kuwa, mwanafunzi analazimika kulipa ada nyingine kwa ajili ya
kozi hiyo.
Said anabainisha kuwa Bodi ya Mikopo, haitoi fedha
kwa ajili ya mahitaji ya kozi maalumu (special falcuty). Anasema kuwa
wanatumia pia fedha zao kwa ajili ya kununua machapisho yanayotolewa na
walimu wao.
“Mwalimu anaandaa kitini cha mazoezi, anatuambia
tununue kwa Sh80,000. Hebu fikiria, tuna kozi 10, kila somo ulipie kiasi
hicho cha fedha, jumla ni shilingi ngapi? Mzazi anatoa wapi pesa ya
kulipa ada na mambo mengine ya darasani?” anahoji mwanafunzi huyo.
Usajili wa chuo na kozi za afya
Rais wa Kitivo cha Sayansi ya Tiba chuoni hapo,
Jackson Raymond anasema wamebaini kuwa hamna kozi yoyote ya afya
iliyosajiliwa na Baraza la Famasia nchini huku wenzao waliomaliza
mafunzo yao chuoni hapo wakinyimwa leseni za ufamasia kwa sababu chuo
hicho hakijapata usajili wa kozi zake.
“Juni mosi, tulimsikia Mwenyekiti wa Kamati ya
Bunge ya Huduma za Jamii, Magreth Sitta akisema chuo chetu bado kina
usajili wa muda mfupi. Tunashangaa ugumu uliopo kwa chuo chetu kupatiwa
usajili wa kudumu,” anasema mwanafunzi huyo.
Anadai kuwa chuo chao pia kinatumia mtalaa wa nje,
kinyume cha Sheria ya TCU, inayotaka chuo chochote kufundisha kwa
kufuata mtalaa wa ndani baada ya kuhakikiwa na tume hiyo au mamlaka
nyingine za afya.
“Sisi tupo hapa kimwili tu, lakini kiakili tuko
Uganda kwa sababu tunachofundishwa hapa ni mtalaa wa Uganda. Tunaomba
Serikali ituhamishie kwenda vyuo vya ndani, vinavyotoa shahada za afya,”
anafafanua Raymond.
Anasema wamefuatilia sehemu mbalimbali kujua
hatima yao, lakini hakuna mafanikio yoyote. Wamekwenda TCU, kwa Mkuu wa
Wilaya ya Ilala, Wizara ya Eimu hata Wizara ya Afya, lakini matatizo yao
bado hayajapatiwa ufumbuzi.
“Hofu yetu kubwa ni hatima yetu baada ya kumaliza
masomo. Tunaweza kuwa hapa baadaye tukaambiwa hatuwezi kupata ajira kwa
sababu tunachokisoma hakijasajiliwa. Sasa tunataka kauli ya Serikali,
isije tukawa tunapoteza muda na fedha zetu nyingi bila sababu ya
msingi,” anasema kiongozi huyo wa wanafunzi na akitaka kujua suluhisho
kwa wanafunzi waliomaliza chuoni hapo.
Gabriel Biseko anasema chuo hicho kimekuwa kikiwataka wanafunzi
wanaofeli mtihani kulipa Sh40,000 kwa ajili ya kurudia mtihani huo wa
‘supplementary’.
Anasema kuwa jambo hilo limekuwa likiwaumiza kwa sababu ya kipato kidogo cha wazazi wao.
“Sijawahi kuona chuo chochote kinalipisha
wanafunzi wake mtihani wa supplementary, ni hapa tu. Serikali imekiacha
chuo hiki kijiendeshe kinavyotaka, sijui TCU wanafanya kazi gani, kama
wanashindwa kusimamia uendeshaji wa chuo hiki,” anafafanua mwanafunzi
huyo.
Biseko anaendelea kusema chuo hicho pia kinatoa
kozi maalumu (bridging course) kwa ajili ya wanafunzi ambao hawakufanya
vizuri katika mitihani yao sekondari. Anaeleza ya kuwa jambo la
kushangaza ni kwamba, hata wanafunzi ambao hawakusoma masomo ya sayansi
wamekuwa wakifundishwa kozi hiyo ya muda mfupi, kisha wanajiunga na chuo
hicho.
Kauli ya KIU
Uongozi wa chuo hicho ulipofuatwa ili kutoa kauli kuhusu madai hayo, ulieleza kuwa haupo tayari kufanya hivyo kwa sasa.
Kauli ya Serikali
Hata hivyo, malalamiko hayo ya wanafunzi,
yanahitimishwa na Serikali baada ya kutembelea KIU, kuzungumza na
uongozi na kutoka kauli.
Juni 10, mwaka huu, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya
Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa alitembelea chuo cha Kampala ili kuzungumza
na uongozi wa chuo hicho pamoja na uongozi wa wanafunzi.
Wanafunzi wa Kitivo cha Sayansi ya Tiba wa chuo
hicho walifika chuoni hapo ili kutaka kuzungumza na waziri huyo licha ya
kuwa walisimamishwa masomo, pia kupigwa mabomu na polisi siku moja
kabla ya ujio wa waziri.
Baada ya mazungumzo na uongozi wa chuo, Dk
Kawambwa alizungumza na wanafunzi hao na kusikiliza madai yao, hoja
kubwa ikiwa usajili wa chuo na kozi za famasia. Hata hivyo, Dk Kawambwa
aliwaondoa hofu wanafunzi na kuwathibitishia kuwa chuo chao kimesajiliwa
kama chuo cha nje sawa na ilivyo kwa vyuo vingine vya aina hiyo.
Alisisitiza kuwa kozi zinazofundishwa katika chuo
hicho, ndizo hizo zinazotolewa pia kwenye matawi mengine ya chuo hicho
yaliyopo nje ya nchi. Alisema kozi hizo zimepitiwa na TCU na
kuidhinishwa kwa sababu zinakidhi matakwa ya mitalaa ya Tanzania.
“Nchi za Afrika Mashariki zimekubaliana kwamba kama programu
zimepitishwa Kenya au Uganda, basi nchi zote za Afrika Mashariki
zitazitambua. Lengo ni kufanya cheti cha mwanafunzi kutambulika pia
maeneo mengine,” alisema waziri huyo.
Dk Kawambwa aliongeza kuwa Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT), kimeanzisha pia matawi katika nchi za Rwanda, Kenya na
Uganda na mtalaa wa Tanzania ndiyo unaofundishwa katika nchi hizo.
Hata hivyo, waziri huyo alisema KIU kimeanza
utaratibu wa kuwa chuo cha ndani na kwamba taratibu zinaendelea na
kitafundisha programu za ndani kama ilivyo kwa vyuo vingine vya ndani.
Kuhusu usajili wa kozi za famasia, Waziri Dk
Kawambwa alitoa barua ya TCU kwenda KIU, kuthibitisha kuwa kozi zote za
famasia zilikuwa zimethibitishwa na TCU tangu Januari 3, 2012.
Kauli ya Nacte
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Elimu ya Ufundi
(Nacte), Dk Primus Nkwera alifafanua kuhusu kozi za muda mfupi na kusema
kuwa kozi hizo ni halali kufundishwa katika chuo chochote kwa sababu
zinamwandaa mwanafunzi kumudu masomo yake.
Hata hivyo, anatahadharisha kuwa kama mwanafunzi
hakusoma masomo ya sayansi O-Level, kozi hiyo haiwezi kumsaidia kwa
sababu inafundishwa kwa muda mfupi kwa aliye na misingi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment