Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Itakumbukwa Agosti 26,1979 Taifa Stars ilikuwa ikihitaji sare ya
aina yoyote dhidi ya Zambia ili ifuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya
Afrika kwa mara ya kwanza tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1968.
Taifa Stars ilikuwa ikicheza mechi hiyo ya
marudiano dhidi ya Zambia kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika za
mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria.
Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha timu hizo,
Taifa Stars iliilaza Zambia bao 1-0 ambalo lilifungwa na kiungo,
Mohammed Rishard Adolph.
Mechi ya marudiano ilichezwa mjini Ndola, nje
kidogo ya jiji la Lusaka na timu ya Zambia ndiyo ilikuwa ya kwanza
kupata bao mwanzoni mwa mchezo, lakini Taifa Stars ilisawazisha bao hilo
mfungaji akiwa Peter Tino.
Bao hilo la Tino lilinyamazisha umati wa mashabiki
wa Zambia waliokuwapo uwanjani kwani liliiwezesha Taifa Stars kufuzu
kushiriki Fainali za Mataifa ya Afrika 1980.
Fainali za Lagos
Baada ya kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa ya
Afrika 1980, katika fainali hizo, Taifa Stars ilichapwa mabao 3-1 na
wenyeji Nigeria katika mechi ya ufunguzi, ilitoka sare ya mabao 2-2 na
Ivory Coast kabla ya kuchapwa mabao 2-1 na Misri na kutolewa hatua ya
makundi.
Kwa miaka 35 sasa, Taifa Stars imekuwa ikisaka nafasi kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika, lakini imeshindwa kuwika.
Fainali za CHAN
Mwaka 2009, Taifa Stars ikiwa chini ya kocha
Marcio Maximo kutoka Brazil ilifuzu kushiriki Fainali za Afrika kwa
wachezaji wanaocheza ligi za ndani ya Afrika (CHAN) baada ya kuichapa
Kenya 2-1 na katika mechi ya marudiano iliichapa tena 1-0. Mechi
iliyofuata Taifa Stars ilicheza dhidi ya Uganda na kushinda 2-0 na
ziliporudiana zilitoka sare 1-1. Mechi ya mwisho Stars iliichapa Sudan
3-1 na ziliporudiana iliibuka na ushindi wa 2-1 na hivyo kufuzu fainali
za CHAN.
Hata hivyo, katika fainali hizo za CHAN, Taifa
Stars ilifungwa na Senegal 1-0, ikaishinda Ivory Coast 1-0 na ilitoka
sare ya 1-1 na Zambia hivyo kutolewa katika hatua ya makundi.
Makocha wa Taifa Stars
(Kocha Marcio Maximo, 2006-2010)
Taifa Stars imekuwa ikinolewa na makocha
mbalimbali wa kigeni na wazawa. Mwaka 2006 ilinolewa na kocha Marcio
Maximo kutoka Brazil ambaye aliiwezesha Stars kushiriki CHAN 2009.
Kingine alichofanikiwa kocha huyu ni kurudisha
ari, moyo na uzalendo kwa wachezaji. Pia Watanzania nao walirudisha moyo
wa kuipenda Taifa Stars, walinunua fulana za kuiunga mkono, walifurika
uwanjani kuishangilia, tulifungwa, lakini tuliridhika na msingi wa soka
ulianza kujengeka chini ya Maximo.
Kocha Marcio Maximo aliiongoza Taifa Stars kuanzia
2006 mpaka 2010 na katika kipindi hicho, Taifa Stars ilicheza mechi 43,
kati ya hizo Taifa Stars ilishinda mechi 16, sare 15 na ilifungwa mechi
12.
Pia Maximo alifanya mapinduzi ya aina yake baada
ya kuipandisha Tanzania kwenye viwango vya Shirikisho la Soka la
Kimataifa (Fifa), kutoka nafasi ya 167 mpaka nafasi ya 108.
(Kocha Jan Poulsen, 2010-2012)
Kati ya mwaka 2010 mpaka 2012, Taifa Stars ikawa
inanolewa na kocha Jan Poulsen raia wa Denmark. Kocha huyu alipokuja
alikuta Watanzania wamehamasika kuipenda timu yao ya taifa na yeye
akaona lipo tatizo ambalo Watanzania wanalifungia macho, tatizo la
kuendeleza mchezo wa soka nchini.
Kocha Jan Poulsen akasema,”Watanzania ndiyo wenye
jukumu la kuendeleza mchezo wa soka nchini hivyo wanatakiwa kutafuta
mfumo thabiti utakaosaidia kufanikisha suala hilo na kuacha mtazamo wa
kuangalia timu ya Taifa tu.”
Poulsen alisema anafahamu suala hilo ni gumu
kutokana na ukubwa wa nchi, kwani rasilimali za kiuchumi zilizopo
zinashindwa kusaidia mchezo wa soka, lakini alisema tunavyozidi
kuchelewa kuusaidia mchezo wa soka ndiyo tunavyozidi kurudi nyuma katika
mchezo huo.
Kocha Poulsen alisema wachezaji wa Kitanzania
anaowachagua Taifa Stars na wanaoendelea kuchaguliwa wanatokana na mfumo
ambao Watanzania wameutengeneza ambao haujali soka la vijana.
Poulsen alisema wachezaji wa Tanzania wanakosa
kufundishwa mambo mengi katika ngazi za chini kwa sababu anaona mambo
mengi aliyokuwa anawafundisha wachezaji kwenye timu ya taifa walitakiwa
wafundishwe wakiwa watoto au vijana.
Katika kipindi hiki ndiyo Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF) likamleta kocha Kim Poulsen kutoka Denmark, ambaye akawa
anazinoa timu za taifa za vijana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) na
miaka 20 (Ngorongoro Heroes).
Jan Poulsen alikuwa na mipango mizuri, lakini ilionekana kushindikana kutokana na uharaka wa Watanzania.
Ni kweli Stars ilishuka kiwango ukilinganisha na kipindi cha Maximo, lakini Jan alikuwa na mipango ya muda mrefu.
Jan alitaka Tanzania iwekeze muda na fedha kuandaa
timu za vijana, miundo mbinu ya soka, kuandaa makocha wenye ueledi wa
juu na kuwa na viongozi sahihi katika nafasi sahihi.
Wakati wa kocha Jan Poulsen, Taifa Stars ilicheza
mechi 22, kati ya mechi hizo, Taifa Stars ilishinda mechi 5, ikatoka
sare 7 na ilifungwa mechi 10. Pia aliiongoza Kilimanjaro Stars ya
Tanzania Bara kutwaa Kombe la Chalenji kwa mara ya kwanza baada ya miaka
16, alipoifunga Ivory Coast kwenye fainali iliyofanyika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
(Kim Poulsen, 2012-2014)
Kocha Kim Poulsen alikuwa akivinoa vikosi vya timu
za taifa za vijana na alipandishwa na kupewa jukumu la kuinoa Taifa
Stars baada ya TFF kumtimua kocha Jan Poulsen.
Alipokuwa anavinoa vikosi vya timu za taifa za
vijana aliweza kuwaibua nyota wengi kama Frank Domayo, Simon Msuva,
Ramadhan Singano, Edward Christopher, Idrissa Rashid ‘Baba Ubaya’,
Hassan Kessy, Atupele Green, Jerome Reuben Lembele, Frank Sekule, Hassan
Dilunga na wengine wengi, ambao baadaye wengine aliwapandisha kuichezea
Taifa Stars.
Kocha Kim Poulsen alikubalika kwa wadau na
wachezaji, Kim alikuwa anawajua wachezaji wa Kitanzania na alikuwa
anatafuta mafanikio yake na Taifa Stars. Kwa wale waliokuwa wanafuatilia
mpira uliokuwa ukichezwa na Serengeti na Ngorongoro walikuwa wanafahamu
ni kocha mwenye uwezo gani. Aliibadilisha pia Taifa Stars ikaanza
kucheza mpira tuliokuwa tunauota, baada ya miaka miwili kupita ya
mkataba wake waliokuwa viongozi wa TFF chini ya rais, Leodeger Tenga
wakampa mkataba mwingine.
Baada ya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya TFF
kufuatia Tenga kumaliza kipindi cha pili cha uongozi, aliyekuja kuchukua
nafasi ya Tenga baada ya uchaguzi alikuwa Jamal Malinzi. Rais huyu mpya
wa TFF alifanya mabadiliko na kumfuta ajira ya kocha Kim Poulsen na
ajira hiyo kumpa kocha Mart Nooij raia wa Uholanzi ili aiwezeshe Taifa
Stars kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2015 jambo ambalo
lilishindikana kwani Nooij alishindwa.
Katika kipindi Kim Poulsen alichoinoa Taifa Stars
ilicheza mechi 15, kati ya hizo Taifa Stars ilishinda mechi 5, ilitoka
sare 4 na ilifungwa mechi 6.
(Kocha Mart Nooij, 2014-2015 )
Kocha Mart Nooij alikuja wakati mbaya kweli kweli,
wakati tunaohitaji matokeo, wakati tunaohitaji kushinda, wakati
tuliokuwa tunahitaji kufuzu kushiriki Fainali za Afrika 2015, hata hivyo
alishindwa kuiwezesha Taifa Stars kufuzu.
Baada ya hapo TFF ilimwambia Mart Nooij kibarua chake
kitasitishwa akishindwa kuiwezesha timu hiyo kufuzu mashindano Afrika
kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2016), tayari kocha Nooij
ametimuliwa jana baada ya Taifa Stars kuchapwa 3-0 na Uganda katika
mechi ya kwanza ya CHAN. Pia benchi la ufundi la Taifa Stars limevunjwa
kuanzia Juni 21, 2015.
Tangu Mart Nooij aichukue Taifa Stars, tayari timu
hiyo imecheza mechi 18 na kati ya hizo imeshinda 3, imetoka sare 6 na
imefungwa 9.
Mitazamo mbalimbali
Mart Nooij anasema,”Mafanikio ya soka yanahitaji
kucheza kitimu ‘Team Work’, kama utakuwa na mabeki wazuri halafu huna
washambuliaji hilo ni tatizo, kama klabu itakuwa na wachezaji wazawa
wazuri kwenye kikosi cha kwanza hakuna shaka timu ya taifa itakuwa nzuri
pia.
“Tatizo jingine baadhi ya wachezaji wanapokuwa
timu ya taifa hawajitumi kama wanavyokuwa kwenye klabu zao, wanashindwa
kung’amua kuwa mazoezi ya timu ya taifa ni ya muda mfupi hivyo wajitume,
lakini wengine wanakuwa wavivu, hilo ni tatizo katika kufanya vizuri,”
anasema Nooij.
Kocha msaidizi wa Yanga, Boniface Mkwasa anasema,
“Taifa Stars inapata kila inachohitaji na mdhamini anajitoa kwa hali na
mali kuhakikisha hakuna kinachokosekana kwa wachezaji na benchi zima la
ufundi, Taifa Stars inapofanya vibaya ni lazima TFF itafute njia za
haraka kutafuta ufumbuzi wa tatizo,” alisema Mkwasa.
Naye kocha wa Yanga, Hans Pluijm anasema, “Katika
mechi dhidi ya Misri, makosa binafsi pamoja na maandalizi ya chini kwa
timu hiyo ndiyo yameigharimu, wachezaji walionekana kama hawajaandaliwa
vizuri kisaikolojia kabla ya pambano lile jambo liliowafanya waonekane
hawajiamini katika muda mwingi wa mchezo.”
Kwa upande wake Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail
Aden Rage amemtaka Rais wa TFF, Jamal Malinzi kumtimua kazi kocha wa
Stars, Mart Nooij kwa kuwa ameshindwa kuivusha Tanzania katika medani ya
soka.
“Kocha wa Taifa Stars ameshindwa kazi, ameonyesha
hawezi, sasa Malinzi ampe chake aondoke, wanamng’ang’ania wa nini?, kila
siku hatuna raha kwa nini? Hata Ulaya, makocha wanatimuliwa kwa
kushindwa kufanya kile kinachokusudiwa,” alisema Rage.
Nyota wa zamani wa Taifa Stars, Sunday Manara
anasema,”Nchi nyingine wachezaji wa zamani wanakuwa karibu na benchi la
ufundi, wanashahuri, lakini Tanzania kitu hiko hakipo, mchezaji wa
zamani hupewi nafasi.
“Tena ukionekana unachangia unaanza kubezwa, hili
ni tatizo, ndiyo sababu kila siku tunazidi kuporomoka badala ya kupanda,
mifumo ya soka letu inapotea,” anasema Manara.
Mkuu wa Idara ya Michezo kwenye Chuo Kikuu cha
Mtakatifu Augustine, Padri Leone Maziku anasema,”Kocha Marcio Maximo
anabakia kuwa pekee ambaye alionyesha mwanga wa kulitoa soka la Tanzania
kutoka hatua moja kwenda nyingine, kocha huyu aliweka msingi imara wa
timu ya Taifa kwa kuwaandaa wachezaji wengi wenye umri mdogo ambao
baadaye waligeuka kuwa lulu Taifa Stars na kwenye klabu zao.
chanzoMwananchi
chanzoMwananchi
0 comments:
Post a Comment