Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Uchukuzi Samuel Sitta.
Uteuzi huo umefanyika kwa mujibu wa kifungu Namba 6 Kifungu kidogo
cha 2 (b) cha Sheria ya Bandari namba 17 ya mwaka 2004 kinachompa
mamlaka ya kuvunja na kuteua wajumbe wa bodi.
Sitta alitangaza uteuzi huo jana jijini Tanga wakati wa ziara ya
kikazi katika Bandari ya Tanga na baadaye kuzungumza na wafanyakazi
waliokusanyika katika uwanja wa Baraka na kusisitiza kuwa mabadiliko
hayo yametokana na vitendo vya uonevu alivyokuta vikiendelea kufanywa
ndani ya TPA.
Wajumbe wapya walioteuliwa ni pamoja na Mhadhiri wa Sheria katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Tulia Akson; Mhandisi wa Ujenzi, Musa
Ally Nyamsingwa; Mtaalam wa Manunuzi na Mjumbe wa Bodi ya Posta, Donata
Mugassa na Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na
Maji (Ewura), Haruna Masebu.
Wengine ni Mhandisi wa Bodi ya Wahandisi Tanzania, Gema Modu;
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Francis Michael;
Mkurugenzi wa Mipango NSSF, Crescentius Magori na aliyekuwa Mkurugenzi
wa Masoko wa TPA, Flavian Kinunda.
Dk. Michael na Akson walikuwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, ambalo Sitta alikuwa mwenyekiti wake.
“Uteuzi huu unatengua uteuzi wa wajumbe wa sasa wa bodi hiyo
kuanzia leo Juni 2, mwaka huu na lengo la uteuzi wa wajumbe hawa ni
kuleta tija na ufanisi wa utendaji kazi ndani ya wa Mamlaka na kwa
nafasi ya Mwenyekiti mpya wa Bodi nasubiri uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete
kwani ndiye mwenye mamlaka hiyo kisheria,” alisema.
Dk. Mwakyembe aliteua bodi ya TPA Novemba 6, 2012.
Mwakyembe aliwateua Dk. Jabir Kuwe Bakari, John Ulanga, Caroline
Temu, Jaffer Machano, Dk. Hildebrand Shayo, Said Salum Sauko, Mhandisi
Julius Mamiro na Asha Nasoro.
Sambamba na hatua hiyo Waziri Sitta aliziagiza taasisi zote zilizo
chini ya wizara ya Uchukuzi ikiwamo Mamlaka ya Hali ya Hewa, Mamlaka ya
Usimamizi wa Anga, Reli na Bandari kuhakikisha wanabuni mifumo mipya ya
motisha ndani ya mamlaka zao ili wafanyakazi wa ngazi za chini wajione
ni sehemu ya mamlaka husika.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment