Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Uuzaji nyumba za serikali, rada, NBC vyamganda, Atamba awamu ya tatu iliimarisha uchumi.
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye, akitangaza nia ya kugombea urais wa Tanzania kupitia CCM jijini Dar es Salaam jana.
Katika mkutano huo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam, aliweka
wazi sababu zilizomsukuma kutangaza nia ya kuwania nafasi hiyo kubwa ya
uongozi wa nchi.
Sumaye ambaye ndiye Waziri Mkuu pekee aliyeshika nafasi hiyo kwa
miaka 10, baada ya kueleza nia yake alipokea maswali ya waandishi wa
habari waliotaka kujua kilichotokea katika uuzwaji wa nyumba za
serikali, sakata la ununuzi wa rada, ubinafsishwaji wa Benki ya NBC,
kuvunjwa kwa jiji la Dar es Salaam na mashamba anayomiliki.
Sumaye akijibu maswali mbalimbali ya waandishi wa habari, alifafanua ifuatavyo:
UUZWAJI WA BENKI YA NBC
Alisema ubinafsishaji wa Benki ya NBC ulifuata taratibu zote kwa
kuwa ilikuwa inajiendesha kwa hasara na ilikuwa na madeni mengi
“Tatizo la NBC wakati ule! sijui watu wanapata wapi taarifa kuwa
NBC ilikuwa inapata faida, nenda ukaulize Hazina ilikuwa inalipa kodi
kiasi gani, hakuna! Benki Kuu (Bot) ndiye ‘regulatory’ wa benki zote
pamoja na NBC…tunakumbuka Gavana wa BoT alitoa tahadhari kubwa kwa NBC
akasema benki hii ina madeni ukipanga noti za Sh. 10,000 zinazidi Mlima
Kilimanjaro,” alisema na kuongeza:
“Hao wanaosema ilikuwa na faida siyo kweli, NBC ilikuwa na hasara
sana na unapouza benki ni sawa na kuuza biashara, NBC ilitangazwa na
siyo kwamba mtu aliitwa akabebembelezwa, waliona haifai na kukabidhiwa
kwa aliyeonyesha unafuu alipewa, walishindanishwa na aliyeshinda
alipewa.”
Alisema siyo mali zake zote za NBC ziliuzwa kwani duka la
kubadilishia fedha za kigeni (Bureau Change) halikuuzwa, iliyouzwa
serikali ilibaki na hisa asilimia 30 na zaidi na kwamba waliangalia
taarifa ya BoT ndiyo wakafanya maamuzi.
“Wapo wanaosema watu walikaa hotelini na kuuziana NBC siyo kweli,” alifafanua.
Inafahamika kuwa awali, thamani ya benki ya NBC ilikuwa ikitajwa kuwa ni takriban Sh. bilioni 28.
Hata hivyo, wawekezaji walipewa kuiongoza na baada ya muda walidai
kuwa NBC haina thamani iliyotajwa awali bali ni Sh. bilioni 15 tu, kiasi
ambacho ndicho hatimaye walikilipa wakati wakiinunua.
Taarifa zaidi zilidai kuwa licha ya kuipata benki hiyo kwa bei ya
chini tena ikijumuisha rasilimali zake kadhaa yakiwamo majengo
yaliyotapakaa katika maeneo mbalimbali nchini, bado wawekezaji hao
waliibua madai ya fedha kutoka benki ya NMB yanayofikia kiasi kilekile
walichonunulia cha Sh. bilioni 15.
Madai hayo yalitokana na matokeo ya ukokotoaji zaidi wakati taasisi hizo zikigawanywa na kuwa mbili tofauti.
Kutokana na hali hiyo (ya NBC kulipwa na NMB kiasi kile kile
kilichodaiwa kutolewa na wawekezaji kuinunua benki hiyo) ndipo
kulipoibuka shutuma mbalimbali kutoka kwa makundi ya wanaharakati dhidi
ya serikali ya awamu ya tatu, yakidai kwamba kilichofanyika kilikuwa ni
sawa na kuitoa bure benki hiyo kwenda kwa wawekezaji.
RADA
Kuhusu kashfa ya rada, Sumaye alisema kwa muda mrefu kumekuwa na
malalamiko juu ya ununuzi wa rada na ndege ya rais na kwamba kuna
tofauti kubwa kati ya uamuzi wa serikali wa kununua na wizi uliobainika
kuwapo ndani ya manunuzi hayo.
Alisema serikali ya awamu ya tatu ililazimika kununua rada kwa kuwa
mashirika makubwa ya ndege yalitishia kuondoa ndege zake katika anga ya
Tanzania na kwmaba kuna wakati Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ndege
aliyokuwa anatumia ilinusurika kugongana na ndege nyingine angani.
“Kama kulikuwa na wizi katika ununuzi wa rada au ndege ya rais hilo
ni suala lingine, kama mtu alifanya faulo huyo tumkamate, usije
ukahusisha watu wengine ambao waliagiza inunuliwe, unafikiri Rais
Mstaafu Benjamin Mkapa au mimi tunajua hiyo rada imefananaje? Kama kuna
mtu alifanya mambo ya ovyo huyo ndiyo tumkamate na ashughulikiwe na siyo
Sumaye,” alisema.
MASHAMBA ANAYOMILIKI
Alisema suala hilo siyo muhimu kwa sasa kwa kuwa siyo Mtanzania
pekee anayemiliki ardhi kubwa nchi hii na kwamba kilichomkwamisha
kuiendeleza ni kushindwa kupata hati kwa kuwa huwezi kuendeleza ardhi
isiyokuwa na hati.
“Iwapo watanipa hati, ardhi yangu niliipata kihalali, nikipata hati
nitatafuta mkopo nitaiendeleza, tuwape moyo viongozi wetu wanaochukua
ardhi kwa njia za hali kwa ajili ya kilimo kuliko kuwaandama, kwani wapo
viongozi wanaoweza kufanya biashara nyingine lakini hazina faida,”
alisema.
UUZWAJI WA NYUMBA ZA SERIKALI
Sumaye alisema kuuza nyumba za serikali ilikuwa ni uamuzi wa
serikali na siyo jambo ambalo lilifanyika nje ya uamuzi wa serikali,
kwani lilipita kwenye Baraza la Mawaziri na kujadiliwa kwa kirefu na
rais akashauriwa akalikubali.
“Sababu kubwa ya kuuza ni kama mnavyojua utawala wa Mzee Mkapa
ulikuwa wa uwazi na ukweli, kuna tume kadhaa zilizofanya kazi juu ya
jambo hili…Tume ya Mramba, Mzee Nsekela, zote zilikuja na mapendekezo
kuwa nyumba za serikali ni nyingi mno, fedha nyingi za serikali
zinaingia katika kutengeneza nyumba lakini bado ni mbovu, hivyo afadhali
serikali ipunguze nyumba zake zibaki chache,” alisema na kuongeza:
“Nyingine zote ziuziwe watumishi na ndivyo tulivyofanya, Kenya,
Uganda wamefanya hivyo, kilichomsukuma rais tulikuwa kwenye
privatization (ubinafsishaji) mashirika ya umma yana maeneo makubwa na
nyumba nyingi, mfano bandari ilikuwa na nyumba zaidi ya 1,000,
ukibinafsisha kama TBL walibinafsishwa na nyumba tukaona tulifanya
makosa, tukaondoa nyumba ndani ya shirika husika kadri inavyowezekana.”
alisema.
Alisema ubinafsishaji kwa ikininafsisha kwa mfumo wa PSRC, nyumba
nyingi zilinunuliwa kwa bei kubwa, na nyingine zilishindikana kuuzwa.
Alisema hata hivyo rais alishtuka kuna maghorofa ‘yanaota’ kwa
wingi eneo la Osterbay na alipouliza ni ya watu gani alielezwa ni zile
zilizobinafsishwa kwa mashirika ya umma.
Sumaye alisema hali hiyo ilimshtua rais ambaye alisema ‘mimi ni
rais ninayetoka Ikulu huku eneo lote la Osterbay hakutakuwa na mwafrika
hata mmoja na kutoa uamuzi wa kuuzwa kwa nyumba za serikali kwa
watumishi wa umma pekee.
Alisema Mkapa alitoa uamuzi nyumba hizo ziiuziwe wafanyakazi
wanaoishi ndani yake na hakuna mfanyakazi atakayeruhusiwa kuziuza ndani
ya miaka 25 ijayo.
“Nyumba zote zilifanyiwa tathmini na ‘Government Value’, watumishi
wakakatwa kwenye mishahara na wengine pensheni na walipewa mikataba ya
miaka 25,” alisema.
SABABU ZA KUGOMBEA URAIS
Sumaye alisema ameamua kugombea nafasi hiyo ya juu ya nchi kwa kuwa
anatambua uongozi wa nchi katika nafasi ya urais ni jukumu zito na
kwamba siyo uamuzi wa kukurupuka bali unahitaji mashauriano ya ndani na
wale anao waamini na kwamba amejipima na kuona anafaa.
“Nimejipima, nimejishauri na nimetafuta ushauri kwa watu wengine
wasema ukweli na mwishowe nimefikia uamuzi wa kugombea nafasi …ni uamuzi
mgumu unaohitaji ujasiri mkubwa kama ni kweli unataka kuwa mtumishi wa
watu kwa maslahi ya watu.
Sumaye ambaye muda mwingi alitumia mafanikio ya serikali ya awamu
ya tatu kujieleza uwezo wake, alisema uamuzi wa kugombea nafasi hiyo
siyo mgumu kama anayetaka kufanya hivyo anakwenda Ikulu kuwa bosi wa
watu na kwa maslahi binafsi au kutaka utukufu au kujitafutia utajiri.
Kuhusu uzoefu, Sumaye alisema amekuwa kiongozi katika ngazi
mbalimbali kuanzia kuwa mfanyakazi wa kawaida wa umma, mbunge, naibu
waziri, waziri na waziri mkuu na kwa kipindi chote hicho alifanya mambo
mengi kwa maslahi mapana ya taifa kwa mafanikio makubwa.
Aidha, Sumaye alisema katika kutekeleza majukumu yake huenda
walifanya makosa ambayo siyo kwa makusudi bali kwa bahati mbaya kwani
katika kila jambo kuna changamoto na kwamba yapo yaliyofanywa kwa nia
njema na kupata tafsiri tata.
Alisema kwa kipindi ambacho amekuwa kiongozi ametembea maeneo
mbalimbali nchini na ameijua vizuri Tanzania na shida na matatizo ya
Watanzania na iwapo atateuliwa hatahitaji kujifunza bali kutenda.
VIPAUMBELE VYAKE
Sumaye alisema kiongozi anayetaka kuwa Rais anapaswa kuwa na sifa kadhaa, zikiwamo 10 alizoziainisha.
Kwa mujibu wa Sumaye, sifa hizo ni kuwa na dira na upeo, kupigiwa
mfano, kujitegemea kifikra na kushaurika, mzalendo wa dhati na
mwadilifu.
Nyingine ni uaminifu, kuijua nchi na wananchi wake, kuongoza kwa
kufuata katiba na sheria, uwezo wa kutofautisha maisha binafsi na ofisi
ya urais, ujasiri usiotiliwa shaka, uwezo wa kuweka na kuisimamia
serikali inayowajibika kwa umma
Sumaye alizitaja sifa nyingine ni kulinda muungano, mshikamano,
amani na utulivu, kujenga na kuimarisha uchumi, kujenga nguzo kuu za
uchumi zilizo imara, kusimamia mapato, matumizi na madeni ya serikali,
kujenga uchumi mpana.
Nyingine ni kuifanya sekta binafsi iongoze maendeleo ya uchumi,
kuweka sera rafiki za uwekezaji kwa wananchi na sekta binafsi na
kuendeleza viwanda ili kuongeza mauzo nje.
Pia, zimo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, kufanya kazi kwa bidii, uaminifu, nidhamu na kuthamini muda, kuboresha.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment