Na Mwandishi Wetu
26/04/2016
Serikali
imeahidi kuboresha Makazi ya watu wenye ulemavu na wenye mahitaji
maalum ili kutatua changamoto wanazokabiliana nazo katika maisha yao ya
kila siku.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye Ulemavu)
Mhe. Dkt Abdallah Possi wakati akichangia hoja katika Mkutano wa Bunge
wa kujadili Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 Bungeni
mjini Dodoma.
Naibu
Waziri aliwaeleza Wabunge umuhimu wa Serikali kuboresha makazi ya Watu
wenye Ulemavu na wenye mahitaji maalum kwa mujibu wa matakwa ya Sheria
ya watu wenye Ulemavu namba 9 ya mwaka 2010 inayoeleza haki za watu
wenye Ulemavu kuboreshewa maeneo muhimu ikiwemo elimu, ajira, fursa sawa
na miundombinu.
“Dhamira
ya Serikali ni kuhakikiasha Watu wenye Ulemavu wanashiriki katika
shughuli mbalimbali kwa kuwawekea mazingira rafiki yanayowasiaida
kutekeleza majukumu yao kulingana na hali zao” Alisema Mhe.Possi.
Aidha,
Serikali imefanya jitihada za awali kwa kuyatembelea makazi ya watu
wenye ulemavu yakiwemo makazi ya Nunge yaliyopo wilaya ya Kigamboni
mkoani Dar es salaam, Sarame Mkoani Manyara, Kituo cha Wagonjwa wa Ukoma cha Msufini mkoani Tanga pamoja na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro
na kubaini umuhimu wa kuyaangalia maeneo hayo ikiwa ni pamoja na
kutatua changamoto za uvamizi wa makazi ya watu wenye mahitaji maalum.
“Makazi
ya watu wenye ulemavu na wale mahitaji maalum yana changamoto nyingi
ikiwemo uchakavu wa majengo, kukosa vifaa, uhaba wa wahudumu, changamoto
za kifedha na uvamizi wa mara kwa mara” Alisema Naibu Waziri.
Naibu
Waziri Possi alisisitiza kuwa hadi sasa Wizara hiyo imeshakubaliana na
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuangalia hatua za
kuzuia uvamizi katika Makazi ya Watu wenye Ulemavu na wenye Mahitaji
maalum ili kuimarisha usalama wao.
Msingi
wa hoja iliyojibiwa na Naibu Waziri imetokana na michango iliyotolewa
na wabunge kuhusu masuala ya Watu wenye Ulemavu kuitaka Serikali
kuhakikisha inaboresha mazingira ya watu wenye ulemavu.
Maeneo
yanayoboreshwa na kutekelezwa ni pamoja na kuwaboreshea namna ya
wanavyotakiwa kupata elimu bora, kukomesha mauaji ya wenye ualbino,
suala la kodi na Makazi ya watu wenye ulemavu na wenye mahitaji maalum
wakati wa kuchangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka
wa fedha 2016/17.
0 comments:
Post a Comment