MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra),
imeanzisha njia mpya ya usafiri wa daladala kati ya Kigamboni na maeneo
mengine jijini Dar es Salaam. Ilianza juzi kutoa leseni kwa mabasi ya
daladala yanayobeba abiria kati ya Kigamboni - Machinga Complex iliyoko
Ilala, Temeke na Mbagala Rangi Tatu.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi ya Mawasiliano ya
Umma ya Sumatra, njia hizo zimeanzishwa kutokana na kufunguliwa kwa
Daraja la Mwalimu Nyerere linalounganisha Kigamboni na maeneo mengine ya
jiji hilo kwa barabara.
Sumatra imewataka wamiliki wa mabasi yanayofanya safari hizo na
wawekezaji katika sekta hiyo kuwasilisha maombi ya leseni katika ofisi
zao mkoa wa Dar es Salaam. Imewataka kuwa na madereva na makondakta
watakaozingatia masharti ya leseni.
Nauli iliyopangwa kati ya Machinga Complex - vituo vya Mpalasingi,
mwanzo wa daraja, getini darajani, JKT, Polisi Ufundi ni Sh 400.
Vilevile kutoka vituo vya Mivinjeni, Bandarini, Keep left na Machinga
Complex nauli itakuwa Sh 450.
Aidha, imeelezwa kuwa nauli itakuwa Sh 400 kwa safari za njia ya
Kigamboni -Temeke kwa vituo vya Mpalasingi, Mwanzo wa daraja, Getini
darajani, Uhasibu, Azizi Ally na Temeke.
Kwa njia ya Kigamboni –Mbagala Rangi tatu, nauli itakuwa Sh 400 kwa
vituo vya Mpalasingi, mwanzo wa daraja, getini darajani, Azizi Ally,
Mtongani . Nauli ya Sh 450 itatozwa kwa vituo vya Msikitini Kizinga,
Misheni, Sabasaba kwa Mpili, Kipati, Kizuiani, Zakhem na Mbagala Rangi
Tatu.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment