Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Flora Mwakasala MAHAKAMA ya Rufaa leo inatarajiwa kusikiliza rufaa
ya kupinga kuachiwa huru kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar
es Salaam (RCO) Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na
askari wenzake wanane waliokuwa wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji.
Rufaa hiyo inatarajiwa kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu
likiongozwa na Jaji Bernard Luanda, wengine ni Jaji Sauda Mjasiri na
Jaji Semistocles Kaijage. Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), alikata rufaa
mwaka 2013, akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam
iliyowaachia huru Zombe na wenzake, baada ya kuwaona hawana hatia katika
kesi ya mauaji ya watu wanne iliyokuwa inawakabili.
Katika rufaa hiyo, DPP anadai kuwa Jaji Salum Massati alikosea
kuwaachia huru washitakiwa hao kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa
kutosha kuwatia hatiani wote. Mbali na Zombe, wajibu rufaa wengine ni
ASP Christopher Bageni, ASP Ahmed Makelle, Konstebo Jane Andrew,
Konstebo Emanuel Mabula, Konstebo Michael Shonza, Koplo Abeneth Salo,
Koplo Rajabu Bakari na Koplo Festus Gwabisabi.
Katika kesi ya msingi inadaiwa Januari 14, 2006, katika msitu wa
Pande uliopo Mbezi Luis, Dar es Salaam Zombe na wenzake waliwaua kwa
makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro, Mathias
Lunkombe, Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi, pamoja na
dereva teksi Juma Ndugu.
Baada ya kusikiliza kesi hiyo, Agosti 17, 2009, Jaji Massati
aliwaachia huru washitakiwa kwa kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa
kuthibitisha mashitaka dhidi yao bila kuacha shaka na Mahakama ikiwaona
hawana hatia kwa makosa yaliyokuwa yanawakabili.
Oktoba 6, 2009, DPP alikata rufaa Mahakama ya Rufani, akipinga hukumu
hiyo kwa madai kuwa Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa
hao, pia kulikuwa na ushahidi wa dhahiri na wa kimazingira unaotosha
kuwatia hatiani washtakiwa wote.
Hata hivyo Mei 8, 2013 Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa hiyo
kutokana na dosari za kisheria zilizobainika kwenye rufaa, lakini DPP
alipeleka maombi Mahakama Kuu ili aruhusiwe kukata tena rufaa nje ya
muda. Mahamaka Kuu ilikubali maombi yake, akakata tena rufaa
inayotarajiwa kusikilizwa leo.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment