Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Kodi toka
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Bi.Rehema Kilonzi akitoa taarifa kwa waandishi wa habari
kuhusu mapato yaliyokusanywa kutokana na
kodi ya pango la ardhi kwa mwaka fedha
2015/2016 ambapo Serikali imekusanya zaidi ya Bilioni 60 kati ya bilioni 70
zilizopangwa.kulia kwake ni mwanasheria toka Wizara hiyo Bw.Seif Hiza na mwisho
ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara hiyo Bi Mboza Lwandiko.
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu mkakati wa Serikali kuwachukulia hatua za
kisheria wananchi waliobadili matumizi ya Ardhi ya makazi na kuyageuza
kuwa maeneo ya biashara na kuisababishia Serikali kukosa mapato
yanayostahili.(Picha na Fatma Salum-Maelezo)
Frank
Mvungi-Maelezo
Serikali imesema itawachukulia hatua
kali za kisheria wananchi waliobadili matumizi ya Ardhi ya makazi na kuyageuza
kuwa maeneo ya biashara na kuisababishia Serikali kukosa mapato ya kodi ya Ardhi.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkuu wa
Kitengo Cha Kodi toka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi.Rehema
Kilonzi wakati akitoa taarifa kwa
waandishi wa habari kuhusu mapato
yaliyokusanywa kutokana na kodi ya pango la ardhi kwa mwaka fedha 2015/2016.
Amesema kuwa baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali
nchini wameyageuza maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya makazi ya watu kuwa nyumba
za kulala wageni,hosteli, maeneo ya biashara kinyume cha Sheria ya Ardhi Namba
4 ya mwaka 1999 chini ya fungu la 33.
“Rai yetu kwa wananchi waliopata fursa
ya kumiliki maeneo yaliyopangwa na kumilikishwa kisheria,tunawaomba walipe kodi
ya Pango la ardhi kwa wakati kuepuka usumbufu wa kufikishwa Mahakamani
.”alisisitiza Kilonzi.
Amesema katika kipindi cha mwaka wa
2015/2016 Serikali imefanikiwa kukusanya kiasi cha Bilioni 60 kutokana na kodi
ya Pango la Ardhi ambazo ni sawa na asilimia 85 ya lengo lililowekwa la
kukusanya shilingi bilioni 70.
Amesema
mkakati wa wizara hiyo ni
kuhakikisha kuwa inafikia lengo la kukusanya Kodi hiyo na kuongeza kuwa hiyo imesambaza maafisa
wake katika Ofisi zote za Kanda ili kuhakikisha kuwa Halmashauri na Manispaa
zinasambaza hati za madai ya Kodi ya pango la Ardhi na kuwafikia wadaiwa wote
kwa wakati muafaka.
Amesema wizara hiyo inaendelea na
mkakati wa kufungua mashauri ili kupata kibali cha mahakama cha kukamata mali
za wadaiwa sugu na kuwapokonya hati
milki katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumzia hatua hiyo amesema kuwa
katika jiji la Dar es salaam mashauri
yataanza kusikilizwa katika Baraza ya Nyumba na Ardhi La Wilaya ya Kinondoni kuanzia
mwezi Mei 2016, kisha zoezi hilo
litaendelea kwa Mikoa na Wilaya zote Jijini hilo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu Kodi ya Ardhi
inayotozwa na wizara hiyo amesema kuwa inatozwa
kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 chini ya fungu la 33.
Amesema kuwa katika kipindi cha mwezi
mmoja na nusu ( kuanzia Februari 2016) Wizara imewafikia wamiliki wa Ardhi 679 katika Maeneo ya Sinza
na Kijitonyama Jijini Dar es salaam na kufanya uthamini wa maendelezo kwa kwa
wale waliokiuka masharti ya matumizi yaliyopangwa ambapo ilibainika kuwa kuna
ukiukwaji wa masharti ya Uendelezaji kwa kubadili matumizi yaliyoainishwa
katika milki zao.
Aidha, amesema kutokana na uthamini uliofanyika mwezi Februari Serikali inatarajia kukusanya jumla ya milioni mia nane kama faini kutokana na ubadilishaji wa matumizi ya maeneo usiozingatia Sheria za Ardhi katika maeneo ya Sinza na Kijitonyama.
0 comments:
Post a Comment