Na: Shamimu Nyaki WHUSM.
Chama cha mpira wa
mikono Tanzania (TAHA) kimetakiwa kufuata sheria na taratibu za usajili wa Katiba
wanayoitaka kama walivyoagizwa na Msajili wa Vyama vya michezo nchini.
Hayo yamesemwa na Afisa
Michezo Mkuu Kitengo cha Usajili wa Vyama vya Michezo Bw. Allen Allex kufuatia
malalamiko ya Chama hicho kwa vyombo vya habari kuwa wamenyimwa usajili wa
katiba mpya ya chama chao.
Amesema kuwa Chama
hicho wakati kinawasilisha barua ya kuomba kusajili Katiba yao aliwapa
utaratibu wa kufuata katika usajili ambao kwanza ni kurudisha Cheti cha mwanzo
cha Katiba ya zamani, pamoja na Orodha ya mabadiliko wanayotaka kuyafanya (Schedule
of Ammendment).
“Lazima waonyeshe
mabadiliko wanayotaka kuyafanya yaliopo katika katiba ya zamani na kuonyesha
wanayotaka kuyaweka katika katiba
mpya”.Alisema Bw. Allen.
Aidha chama hicho
kinatakiwa kufanya mkutano mkuu wa mabadiliko ya Katiba chini ya sheria ya
Usajili wa Vyama vya Michezo ya Baraza
la Michezo la Taifa (BMT) ambayo inaeleza kuwa ni lazima mkutano kuwa na
wajumbe wa vyama vya michezo kutoka mikoa
isiyopungua 13 ya Tanzania Bara.
Kutokana na masharti
hayo chama hicho hakikuweza kutimiza na badala yake wakafanya mkutano na
wajumbe ambao sio sahihi kisheria.Chama hicho Tarehe
17/12/2015 kiliwasilisha barua ya kuomba usajili wa
Katiba mpya ambayo ilikuwa inataka kubadilisha jina la chama hicho kutoka
Tanzania Ameteur Handball Association (TAHA) na kujulikana kama Shirikisho la
la Mpira wa Mikono la Tanzania (THI).
0 comments:
Post a Comment