Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Lilian Lundo – Maelezo
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar
es Salaam limeazimia kuongeza idadi ya madampo na kurekebisha
miundombinu ya dampo la Pugu ili kuhakikisha jiji linakuwa safi.
Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es
Salaam Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Isaya Mwita alisema
Baraza hilo limeazimia kuongeza na kurekebisha miundombinu baada ya
ziara walioifanya na kugundua mapungufu katika dampo la Pugu.
“Tumegundua kuna udhaifu mkubwa katika dampo la
Pugu, magari yanayopeleka taka yananasa barabarani hivyo tukaona kuna
sababu ya kutengeneza miundombinu, hivyo tumetenga milioni 700 kwenye bajeti hii ili kutengeneza barabara hiyo,”alisema Mhe. Mwita.
Aidha, alisema kwamba baraza limetenga kiasi cha
shilingi milioni 200 katika bajeti ya 2016/17 ili kununua eneo Mkuranga
kwa ajili ya dampo, huku wakiendelea na mchakato wa kuongeza madampo
mengine Kigamboni na Kisarawe ili kuhakikisha taka zote zinazozalishwa
ndani ya jiji la Dar es Salaam zinapelekwa kwenye madampo badala ya
kuzagaa mitaani.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa jiji la Dar es
Salaam Mhe. Mussa Kafana alisema kuwa, suluhisho la kumaliza taizo la
uchafu si kuwa na dampo tu bali ni kuwepo kwa vifaa maalumu vya
kuhifadhi taka. Hivyo baraza likaamua kuwepo na vyombo vya kuhifadhia
taka katika mitaa yote ya jiji la Dar es Salaam ili kudhibiti uzagaaji
wa taka.
Usafi ni moja ya kipaumbele cha Rais wa Awamu ya
Tano Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ambapo kwa mara ya kwanza alitangaza
siku ya Uhuru wa Tanzania (Tisa Desemba) iazimishwe kwa kufanya usafi
nchi nzima ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu
pamoja na kuiweka Tanzania katika hali ya usafi.
0 comments:
Post a Comment