Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro
WATU wawili wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameuawa na mwingine
mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kujihusisha na ujambazi jijini
Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam Kamishna wa Polisi Kanda
Maalumu Dar es Salaam, Simon Sirro wakati akizungumza na waandishi wa
habari.
Alisema tukio hilo lilitokea Mei 28 mwaka huu baada ya polisi kupata
taarifa kuwa maeneo ya Mburahati kuna majambazi watatu, ambao walikuwa
wanafukuzwa na kundi la bodaboda huku wakifyatua risasi.
Sirro alisema katika ufuatiliaji askari walifika katika eneo hilo na
kukuta jambazi mmoja akishambuliwa na wananchi baada ya silaha aliyokuwa
akiitumia kuishiwa risasi.
Jambazi huyo alikutwa na silaha moja, bastola LLA yenye namba 649440.
Alisema majambazi wengine wawili, walikimbia wakiwa na bodaboda yenye
namba za usajili MC 444 BFY.
Polisi waliwakimbiza wakishirikiana na madereva bodaboda hadi kufika
katika eneo la Kisukuru, ambako majambazi hao walianguka na kuangusha
bastola yao aina ya Chinese Star, ndipo wananchi walianza kuwashambulia
kwa mawe na fimbo.
Aliongeza kuwa majambazi hao, walishambuliwa baada ya muda mfupi
walifariki dunia huku mwingine alifanikiwa kukimbia na begi dogo jeusi
lililokuwa na fedha.
Sirro alisema awali majambazi hao, walikuwa watatu wakiwa kwenye
pikipiki maeneo ya Buguruni, ambapo walifanya tukio la uporaji wa Sh
500,000 mali ya Mushi Bakari, aliyekuwa na gari namba T 786 CZI Toyota
IST ambaye walimjeruhi mkono wa kulia.
Katika tukio jingine, jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtu mmoja
anayetuhumiwa kuwa jambazi huko Temeke akiwa na bastola Glock P241 yenye
namba NK 172374 ikiwa na risasi 14 ndani ya magazini.
Alisema jambazi huyo alikamatwa baada ya kufanya tukio la uporaji
maeneo ya Chang’ombe Maduka Mawili ya Tigo Pesa akiwa na mwenzake,
ambapo walikimbia kwa kutumia pikipiki.
Chanzo Gazeti La Habari Leo
0 comments:
Post a Comment