Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » SERIKALI YAENDELEA NA MPANGO WA KUSOGEZA HUDUMA ZA AFYA VIJIJINI.

SERIKALI YAENDELEA NA MPANGO WA KUSOGEZA HUDUMA ZA AFYA VIJIJINI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Na Fatma Salum- MAELEZO, Dodoma.


Serikali imewahakikishia wananchi kuwa inaendelea na utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa zahanati kila kijiji, vituo vya afya kila kata na Hospitali katika kila Wilaya ikiwa ni mkakati wake wa kuboresha huduma za afya kote nchini.

Hayo yamesemwa leo bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleiman Jafo wakati akijibu swali la Mbunge wa Busokelo Mhe. Fredy Mwakibete kuhusu Mpango wa kujenga zahanati kila Kijiji na kituo cha afya kila Kata. 

Mhe. Jafo alisema kuwa Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi inaendelea na ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na Hospitali kila Wilaya ambapo ujenzi huo unafanyika chini ya Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM).

“Utekelezaji wa Mpango huo unaendelea na kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri zimetengewa shilingi bilioni 182.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya na kipaumbele kitatolewa katika kukamilisha miradi viporo badala ya kuanzisha miradi mpya.” alisema Jafo.

 Kwa mujibu wa Mhe. Jafo, Ofisi ya Rais TAMISEMI inafanya tathmini ya utekelezaji wa mpango wa MMAM ili kujua idadi ya Vijiji ambavyo havina zahanati, Kata ambazo hazina vituo vya afya na Wilaya ambazo hazina Hospitali lengo likiwa ni kuhakikisha maeneo hayo yanapewa kipaumbele na kutengewa fedha ili kusogeza huduma za afya karibu na wananchi.

Akieleza mafanikio ya mpango wa MMAM, Mhe. Jafo alisema kuwa chini ya mpango huo vituo vya kutolea huduma za afya vimeongezeka kutoka 5,255 mwaka 2006/2007 hadi 6,935 mwaka 2014/2015 sawa na ongezeko la asilimia 39.9 hivyo kuna matumaini makubwa ya kuvifikia vijiji vingi kupitia mpango huo.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa