Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Serikali
imewatoa hofu na kuwahakikishia Watanzania na abiria wanaotumia usafiri
wa anga nchini kwamba mafuta ya ndege yapo ya kutosheleza matumizi kwa
muda wa siku 14 wakati shehena nyingine za mafuta hayo zinaendelea
kuingia nchini.
Hayo
yamesememwa na Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo
alipofanya ziara leo jijini Dar es salaam kukagua matanki ya kuhifadhia
mafuta ili kujionea hali ya upatikanaji wa mafuta ya ndege nchini baada
ya kugundua baadhi ya shehena ya mafuta hayo yaliyoingizwa nchini
yalikuwa yamechanganyika na mafuta ya petroli.
“Mafuta
ya ndege yapo na ndege zitaendelea kufanya safari kama ratiba zao
zilivyopangwa na Watanzania msiwe na wasiwasi, tumejiridhisha, mafuta
yanatosheleza kwa muda wa siku 14 wakati hatua ya shehena nyingine
kuingia nchini zinaendelea” alisema Prof. Muhongo.
Ziara
hiyo ya Waziri Prof. Muhongo inafuatia kugundulika kwa mafuta ya ndege
yaliyoingizwa nchini mapema mwezi Mei mwaka huu, ambayo hayafai kwa
matumizi yaliyokusudiwa kutokana na kuchanganywa na mafuta ya petroli.
Aidha,
Prof. Muhongo ameitaka kampuni ya Sahara Energy Resources yenye makao
yake makuu nchini Nigeria ambayo ndio ilioingiza mafuta hayo nchini,
kusimamisha shughuli zake mara moja hadi suala hilo litakapopatiwa
ufumbuzi.
Imeonekana
si mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuingiza mafuta machafu nchini,
hatua iliyomfanya Waziri huyo kuchukua msimamo huo wa Serikali hadi
suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
Akizungumzia
hatua hiyo na hali ya mafuta nchini, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Wakala
wa Uingizaji Mafuta kwa Pamoja nchini, Michael Mjinja amesema kuwa
mafuta ya ndege yapo na yanatosheleza kwa wiki mbili kuanzia sasa.
Mjinja
aliongeza kuwa wanakuhakikisha uhaba wa mafuta hayo hautokei tena
nchini ambapo wanaendelea kushirikiana na kampuni ya Total na SP Rwanda
ambazo hadi sasa ndio zenye mafuta safi yanayokubalika kwa matumizi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya TIPER iliyoko eneo la
Kigamboni jijini Dar es salaam, Stephane Gay amesema kuwa kampuni yake
ina nafasi ya kutosha ya kuyahifadhi mafuta yote ambayo hayastahili
kutumika ili matanki na mitambo ya kampuni zote zilizopata mafuta hayo
yafanyiwe usafi upya tayari kwa kuweka mafuta safi yanayoingia nchini.
Ziara
ya Waziri Prof. Muhongo imehusisha kutembelea matanki ya kampuni tano
za mafuta ikiwemo Puma, GAPCO, Oil Com, TIPER pamoja na Kampuni ya Oryx
Energies.
0 comments:
Post a Comment