Home » » Serikali kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo

Serikali kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa
SERIKALI imesifu kazi nzuri inayofanywa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini (CRB) na imeahidi kutenga miradi mikubwa ya ujenzi na kuwapa kwa upendeleo makandarasi wazalendo kama hatua ya kuwajengea uwezo.
Ahadi hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipokuwa akifunga mkutano wa siku mbili ulioandaliwa na Bodi ya Makandarasi (CRB), mkutano ambao awali ulifunguliwa na Rais John Magufuli.
Alisema Serikali ina wajibu wa kuwajengea uwezo makandarasi wazalendo kwa sababu hakuna mgeni atakayekuja kuwasaidia Watanzania.
Aliwataka makandarasi kutumia fursa hiyo kujenga miundombinu imara na kwa ubora wa hali ya juu ili miradi hiyo iendane na thamani ya fedha zilizotolewa katika mkataba.
Alisema maono ya serikali ya awamu ya tano ya kujenga miundombinu bora na imara na hayawezi kufanyika bila kuwa na makandarasi wazalendo wenye uwezo wa kuitekeleza kwa viwango vya hali ya juu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Makandarasi, (CRB), Consolata Ngimbwa, alisema Bodi haitasita kuwachukulia hatua kali makandarasi ambao watapewa kazi na kuzifanya chini ya kiwango.
Alisema kila mkandarasi anapaswa kutekeleza mradi wake kama mkataba baina yake na mteja wake unavyotaka na ahakikishe thamani ya fedha zilizotolewa kwenye mradi hiyo inaonekana.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Joseph Nyamhanga, alisema ili makandarasi wazalendo waendelee kuaminika lazima wakamilishe miradi kwa wakati na kwa ubora wa hali ya juu.
“Rais Magufuli anaposema anachukia rushwa huwa hatanii na ndiyo maana wakati anafungua alikuja na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, kwa hiyo suala la rushwa kwenye sekta hii si la mzaha tutapambana nayo kwelikweli,” alisema Nyamhanga Nyamhanga.
Chanzo Kutoka Habari Leo

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa