Frank Mvungi-MAELEZO
Serikali imewataka
wauzaji wa vifaa vya Mawasiliano vya mkononi (mobile devices) kuacha mara moja
tabia ya kubadilisha namba tambulishi (‘kuflash’) za vifaa hivyo kwani watakabiliwa na kifungo kisichopungua miaka
10 au faini isiyopungua milioni 30 au vyote viwili.
Kauli hiyo
imetolewa na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka
ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Innocent Mungy wakati wa mkutano na
waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam.
“Namba
tambulishi (IMEI) za vifaa vyote vya
Mawasiliano ya mkononi ambavyo vimeibiwa,vimeharibika,kupotea au visivyokidhi
viwango vya matumizi katika soko la mawasiliano havitaruhusiwa kuunganishwa
kwenye mitandao ya watoa huduma ifikapo tarehe 16 June 2016. “Aalisema Mungy.
Akizungumazia
kampeni ya kuelimisha umma kuhusu matumizi ya simu zote zisizokidhi viwango,
Mungy alibainisha kuwa idadi ya simu
hizo imeshuka kutokana na elimu ambayo wameitoa katika mikoa mbalimbali hapa
nchini.
Alisema lengo la elimu hiyo kwa umma ni kujenga uwezo
kwa wananchi kutambua simu zisizokidhi vigezo kabla ya kufika ukomo wa matumizi
ya simu bandia nchini.
Mungy
alifafanua kuwa uchambuzi wa IMEI unaonyesha kuwa hadi Februari,2016 idadi ya namba tambulishi ambazo zilikuwa
hazina viwango zilikuwa sawa na asilimia 3 ambapo namba tambulishi ambazo
zimenakiliwa zilikuwa sawa na asilimia 18 na simu halisi zilikuwa sawa na
asilimia 79.
“Kwa
mwezi Machi 2016 ulionyesha kuwa Idadi ya namba tambulishi ambazo hazina
viwango ni asilimia 4, na idadi ya zile zilizonakiliwa zilikuwa sawa na
asilimia 13 ambapo uchambuzi huu umehusisha taarifa za kampuni zote za simu
nchini’’. Alifafanua Mungy.
Aliongeza
kuwa matokeo hayo mazuri ni matunda ya ushirikiano mzuri uliopo kati ya Mamlaka
hiyo, Shirika la viwango Tanzania (TBS),Tume ya ushindani (FCC),kampuni za
simu, pamoja na wadau wengine katika kuelimisha umma juu ya uhakiki wa simu
walizo azo ikiwa ni pamoja na mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kununua simu
ikiwemo kuzihakiki ubora wake.
Kwa Upande
Wake Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Injinia Gabriel Mruma
amesema kuwa ni vyema watanzania wakajenga utamaduni wa kununua simu zenye ubora kuepuka usumbufu wakati Tanzania
inapoelekea ukomo wa matumizi ya simu bandia.
Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania ni Taasisi ya Serikali yenye Dhamana ya kusimamia shughuli
za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta hapa nchini.
Kuwepo kwa
Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 na Kanuni
zake za mwaka 2011 kumewezesha kutekelezwa kwa mfumo wa rajisi ya namba za
Utambulisho wa vifaa vya mawasiliano vya mkononi.
Mfumo huu wa
kielektroniki ulizinduliwa tarehe 17 Desemba 2015 na unahifadhi kumbukumbu za
namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi kwa lengo la kufuatilia
namba tambulishi za vifaa vilivyoibiwa,kuharibika au kupotea,bandia vya
mawasiliano katika soko.
0 comments:
Post a Comment