Home » » TUZILINDE HAKI ZA BINADAMU.

TUZILINDE HAKI ZA BINADAMU.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Na Benedict Liwenga-MAELEZO.

Tanzania imechukua hatua kadhaa za kulinda na kuhifadhi haki za binadamu nchini. Hatua hizo zinajumuisha kuridhia mikataba kadhaa muhimu ya Kimataifa na Kikanda ya haki za binadamu, kuingiza baadhi yake kwenye sheria za nchi na kuanzisha Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB).

Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha Mahakama, Bunge na Vyombo vyote vinavyosimamia utekelezaji wa Sheria nchini.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya Azimio la Vienna la mwaka 1993 na Programu yake ya utekelezaji, kila serikali ulimwenguni inapaswa kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu, ambapo kwa upande wa Serikali ya Tanzania iliamua kuanzisha mchakato huu.

Mnamo mwaka 2009, THBUB iliongoza warsha ya Kitaifa ya Mashauriano yenye lengo la kuandaa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Haki za Binadamu ambapo warsha hiyo ilijumuisha wajumbe mbalimbali kutoka Serikalini, Wanataaluma, Asasi za Kiraia pamoja na Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN).

Mpango Kazi huu unajumuisha mapendekezo mengi ya kimataifa na unatoa mwongozo wa utekelezaji ulio wazi kwa Wizara mbalimbali katika kukuza haki za binadamu nchini. Unaelezea malengo ya jumla na hatu za msingi zinazopaswa kuchukuliwa huku ukibainisha Wizara zinazohusika.

Aidha, Mpango huu unajumuisha Mfumo wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) wenye viashiria vinavyopimika, ambao pia unaimarisha utekelezaji wa Mpango Kazi.

Mpango Kazi huu utaimarisha haki za binadamu nchini Tanzania kupitia baadhi ya malengo yakiwemo kufanya tathmini kuhusu masuala ya haki za binadamu na kuandaa mikakati ya kukuza utoaji elimu ya haki za binadamu na kuongeza uelewa kwa Watanzania wote.

Halikadhalika, Mpango umebainisha haki 23 zilizoko katika makundi manne ya kimada kama maeneo ya kipaumbele katika kuimarisha ukuzaji na ulinzi wa haki za binadamu nchini. Haki na makundi hayo yanajumuisha Haki za kiraia na Kisiasa, Haki za kiuchumi, Kijamii na Kiutamaduni, Makundi yenye Mahitaji Maalumu, Kuimarisha Taasisi na Msuala yaliyopo ambapo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ikisaidiwa na Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itafuatilia utekelezaji wa Mpango huo.

Pamoja na hayo, haki za binadamu nchini zina changamoto kadha wa kadha zikiwemo; Uelewa mdogo wa haki za binadamu nchini ambapo bado ni mdogo haswa katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mjini na hali hii inaathiri kiwango cha utoaji taarifa za uvunjifu wa haki za binadamu, utoaji taarifa wa vyombo vya habari na uwezo wa asasi za kiraia kwa ujumla.

Changamoto nyingine ni tabia ya ubaguzi ya baadhi ya watu wanaotoa huduma, Ukatili dhidi ya wanawake, hatari kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na nyinginezo.

Ili kushughulikia changamoto hizi, Mpango Kazi wa Kitaifa wa miaka mitano wa Haki za Binadamu 2013-2017 uliozinduliwa Desemba 10, 2013 unaainisha hatua za kiutendaji zitakazoiwezesha Serikali ya Tanzania kutekeleza Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu na kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinaheshimiwa nchini kote.

Wakati Tanzania inaelekea kufanyiwa Tathmini ya Awamu ya Pili na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa (UN) juu ya utekelezaji wa haki za binadamu, Asasi za Kiraia pamoja na Taasisi za kutetea haki za binadamu nchini zimeendelea kujadili kuhusiana na haki hizo ambapo Waandishi wa Habari nchini wanaaswa pia kujikita katika kuhabarisha umma kuhusiana na masuala ya haki hizo hususani masuala ya mauaji ya watu wenye ualbino, mauaji ya vikongwe, ukatili dhidi ya watoto, pamoja na adhabu ya vifo.

Miongoni mwa masuala hayo ndiyo yanakamilisha idadi ya mapendekezo 46 yaliyobakia kusainiwa na Tanzania ambapo Mshauri wa masuala ya haki za binadamu kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Bi. Chitralekha Massey anaeleza kuwa, ni vema Tanzania ikakubalina na mapendekezo yanayohusiana na masuala ya haki za binadamu yanayoendana na Dunia kwa ajili ya ulinzi wa haki hizo.

“Sisi kama Umoja wa Mataifa tunapenda kuona Tanzania inafanya uamuzi utakaosaidia kuboreshwa kwa haki za binadamu nchini kwani ni wakati sasa wa jamii kusema kwa uwazi kuwa mapendekezo hayo yatakuwa yenye manufaa kwao”, alisema Massey.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika hivi karibuni mkoani Morogoro, masuala ya haki za binadamu yanazungumzwa kwa upana lengo likiwa ni kuwajengea wanahabari uelewa wa kutosha kuhusiana na masuala ya haki hizo ili wao waweze pia kuhabarisha umma.

Kamishna wa Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi. Salma Ally Hassan anatoa rai kwa waaandishi wa habari huku akiwasisitizia kuwa hawanabudi kujitahidi kuandika habari kuhusu haki za binadamu kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wameisaidia jamii kupata uelewa wa masuala hayo.

Bi. Salma alisema kuwa, baadhi ya wanajamii wamekuwa hawazitambui baadhi ya haki zao hali iliyopelekea kukithiri kwa vitendo vya uvunjifu wa amani yakiwemo matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino, vikongwe pamoja na ukatili kwa watoto nchini.

Aliongeza kuwa, baadhi ya watu nchini wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi kwa kuua watu ovyo ambapo watu wenye kuyasemea hayo ni Vyombo vya Habari lengo likiwa ni kukemea hali hiyo ili vitendo hivyo visiendelee tena katika jamii.

“Uvunjaji wa haki za binadamu unafanywa na watu waliomo katika jamii zetu, kwa mfano, mauaji ya Watu wenye Ualbino, mauaji ya Vikongwe, pale sio Serikali inakua imevunja haki za binadamu, bali ni watu katika jamii”, alisema Bi. Salma.

Aidha, katika warsha hiyo, moja ya mada zilizojadiliwa ni namna gani Vyombo vya Habari, jamii pamoja na Serikali vinakuwa na jukumu la kulinda haki za binadamu na kuendelea kukemea matukio yanayovunja amani katika jamii.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 9 Mei, 2016 Tanzania inatarajiwa kufanyiwa tathmini ya pili juu ya hali ya haki za binadamu nchini na Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa ambapo tayari Asasi za Kiraia na Watetezi wa haki za binadamu wamekwisha wasilisha mapendekezo yao kwa Wawakilishi wa nchi wanachama wa umoja huo.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa