(Picha zote na Benedict Liwenga)
Na Benedict Liwenga-MAELEZO.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
imepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 ikiwa ni
sehemu ya mkakati wa kutoa chanjo kwa akina mama na watoto dhidi ya magonjwa
mbalimbali nchini.
Akiongea na waandishi wa habari Wizarani hapo, Mkurugenzi wa
Huduma za Kinga, Dkt. Neema Rusibimayila ameeleza kuwa vifaa tiba hivyo vitasaidia
uhifadhi wa chanjo katika mikoa mbalimbali pamoja halmashauri nchini.
‘’Ni msaada mkubwa tulioupata toka WHO na nina amini kuwa
utatusaidia sana katika kufanikisha suala la chanjo kwa akina mama na watoto nchini
na pia tunaamini wataendela kushirikiana na Wizara ili tuweze kufikia malengo
tuliyojiwekea’’, alisema Dkt. Rusibimayila.
Ameongeza kuwa, kwa sasa vituo vipya vinavyofunguliwa nchini vikiwemo
vile ambavyo havikuwa na majokofu vitakuwa na uwezo wa kupata vifaa hivyo kama
vile majokofu na vifaa vingine vya tiba ili huduma za chanjo ziweze kutolewa
katika kila kituo nchini.
Akikabidhi vifaa hivyo Wizarani hapo, Mwakilishi wa Shirika
la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania Dkt. Rufaro Chatoro amesema kuwa vifaa hivyo vyenye thamani ya
shilingi bilioni 1.4 ni pamoja na majokofu 200 pamoja na vifaa vitumikavyo kwa
ajili ya kutolea chanjo.
Kwa upande wake Mratibu Chanjo Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bwana Emmanuel Yohana ameeleza kuwa, majokofu
hayo pia yatapelekewa katika wilaya ambayo yana upungufu wa majokofu pamoja na
vituo vipya kwa ajili ya kupunguza umbali kwa wagonjwa wa chanjo na pia ni moja
ya kuweka huduma karibu na wananchi nchini.
Aidha, ameongeza kuwa spesimeni za polio na surua zilizotolewa
na WHO zitapalekwa pia katika vituo kwa jili ya kuchukua damu kwa ajili ya
vipimo na kuletwa Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi wa maabara.
‘’Wanufaika wa huu msaada kutoka WHO ni wananchi wote wa
Tanzania kwani utaenda katika vituo vyote vya chini zikiwemo Zahanati’’,
alisema Yohana.
Kupitia wadau mbalimbali Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kushirikiana na wadau hao katika kutafuta
vifaa tiba mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kuwa sekta ya afya nchini
inaimarika kwani Tanzania kwa sasa imeweza kudhibiti polio kwa kiasi kikubwa.
0 comments:
Post a Comment