Na Eliphace Marwa MAELEZO
Jeshi la polisi Mkoa wa kipolisi Ilala limewahakikishia usalama wananchi wa Mkoa wa kipolisi Ilala na kuachana na taarifa za uvumi kuhusu hali ya usalama katika mkoa huo wa kipolisi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lucas Mkondya amesema
kuwa Jeshi la Polisi limejipanga ipasavyo kukabiliana na uhalifu wa
aina yoyote na kutoa tahadhari kwa wahalifu kuwa makini kwani jeshi lake
limejidhatiti ipasavyo.
“Niwahakishie
wananchi kuwa hali ya ulinzi iko vizuri na jeshi la polisi Mkoa wa
Ilala limejipanga vizuri hivyo wananchi wawe na amani kwani tunafanya
kazi usiku na mchana ili kuhakikisha hali ya amani na utulivu inakuwepo
wakati wote”, alisema Kamanda Mkondya.
Aidha
kuhusiana na malalamiko ya wananchi wa Buguruni kuhusiana na kuwepo kwa
kundi la vibaka na waporaji kamanda Mkondya amesema kuwa Jeshi lake
linaendelea na operesheni ya kukamata wahalifu usiku na mchana ili
kuhakikisha Mkoa wa kipolisi wa Ilala unakuwa salama ambapo mpaka sasa
jeshi hilo linawashikilia baadhi ya wahalifu waliokuwa vinara wa uporaji
eneo la Buguruni Chama.
“Mpaka
sasa tunawashikilia vijana kadhaa ambao walikuwa ni kero katika eneo la
Buguruni chama na maeneo mengine ya Mkoa wa Ilala”, aliongeza Kamanda
Mkondya.
Kwa
upande wake Afisa habari wa Manispaa ya Ilala Bw. David Langa amesema
kuwa Manispaa yake kwa kushiriana na Jeshi la Polisi wako katika mkakati
wa kuanza operesheni ya kuwaondoa wapiga debe ambao wamekuwa
wakishtumiwa na wananchi kujihusisha na vitendo vya uhalifu katika
sehemu mbalimbali za Manispaa ya Ilala.
Aidha Kamanda Mkondya amewataka wakazi wa Ilala kutoa taarifa za kihalifu kwa jeshi lake ili kuweza kuifanya Ilala kuwa salama na kutimiza dhana ya ulinzi shirikishi.
0 comments:
Post a Comment