Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com
Home » » Wakurugenzi wa Halmashauri watakiwa kujipanga na kukamilisha miradi ya ULGSP.

Wakurugenzi wa Halmashauri watakiwa kujipanga na kukamilisha miradi ya ULGSP.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 


Wakurugenzi wa Halmashauri zinazotekeleza mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania( ULGSP) wametakiwa kuangalia maeneo yote yanayokwamisha utekelezaji wa mradi na kuyafanyia kazi kwa kuyaboresha ili kuweza kwenda sambamba na muda uliopangwa kukamilisha utekelezwaji wa mradi huo.
Akifungua Mkutano wa siku tatu wa kufanya mapitio ya utekelezaji wa  Mradi wa  Uboreshaji Miji Tanzania jijini Arusha, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhandisi Mussa Iyombe alisema katika mkutano amegundua kuwa utekelezaji wa mradi wa ULGSP umechelewa kutekelezwa na hivyo aliwataka Wakurugenzi kuangalia maeneo yanayokwamisha utekelezaji na kuyatafutia ufumbuzi ili mradi uweze kukamilika kwa wakati.
“ Katika mkutano huu nimegundua kuwa bado tupo nyuma, tumechelewa katika utekelezaji hivyo ninaagiza katika mapitio ya mradi yanayofanywa, kuondoa vikwazo vyote vinavyotuchelewesha ili tuweze kufikia malengo katika miaka miwili ya utekelezaji wa miradi iliyobakia”Alisema Mhandisi Iyombe.
Alisema ana Imani kuwa vikwazo vikiondolewa na mradi kutekelezwa vizuri Benki ya Dunia itatoa fedha nyingine ya kufanyia kazi katika awamu nyingine ya programu  na hatimaye mradi huu kuweza kufanyika kwenye halmashauri zingine.
Akiwasilisha mada katika kikao hicho Mkurugenzi wa Mipango Miji wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Hante alisema yapo mambo kadhaa yaliyopelekea miradi ya Uboreshaji Miji Tanzania kukwama yakiwepo masuala ya ucheleweshwaji wa fedha pamoja na mchakato wa upitishaji wa fedha za manunuzi.
Katika kutatua changamoto moja ya chanagamoto iliyokuwa ikizikabili halmashauri katika mchakato wa manunuzi, Serikali sasa imeruhusu Halmashauri katika vikao vyake vya kisheria kupitisha fedha isiyozidi bilioni moja badala ya Shilingi milioni 50 iliyoruhusiwa awali.
Awali kabla serikali haijabadili sheria ya manunuzi halmashauri zilitakiwa kuomba kibali cha kupitisha fedha za matumizi zinazozidi milioni 50 kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali hali ambayo ilipelekea kuwepo kwa ucheleweshwaji wa utekelezaji wa mradi.
Wakizungumza katika kikao hicho baadhi ya Wakurugenzi walioshiriki katika mkutano huo wa mapitio wamepongeza hatua iliyofanyika katika  kuboresha mchakato wa manunuzi  kwa kuruhusu Halmashauri kwa kupitia vikao husika kupitisha fedha isiyopungua bilioni moja badala ya Tsh. Milioni 50 iliyokubaliwa awali.
"Awali Wakurugenzi walipata taabu kusimamia miradi mbalimbali katika halmashauri zetu kwasababu  mchakato  wa  sheria za manunuzi, lakini hivi sasa miradi inayofadhiliwa na benki ya Dunia itatekelezwa kwa wakati kutokana na serikali kurahisisha mchakato huu wa manunuzi ". walieleza.
Akifungua mkutano huo  Katibu Mkuu Ofisi ya  Rais-TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe aliwasihi Wakurugenzi wa Halmashauri 18 ambazo zinatekeleza mradi wa ULGSP kuhakikisha wanatumia fursa hiyo  kuleta maendeleo kwa wananchi pamoja na kuainisha vipaumbele vya miradi  ili kutatua changamoto zilizokuwa zikiwasumbua wananchi kwenye halmashauri zao.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita Bwana Marx Kamaoni aliishukuru serikali kwa kuwezesha kuiboresha sheria hiyo ya manunuzi kwani awali mradi huo ulianza mwaka 2013 lakini ulikumbana na changamoto mbalimbali katika sekta ya manunuzi  ingawa licha ya changamoto hizo halmashauri hizo 18 zilishaanza kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara, vituo vya mabasi, vituo vya malori, machinjio na ukarabati wa sehemu za utupaji wa taka ngumu.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Songea Bibi Jenifa Omolo alisema mradi wa ULGSP umeleta maendeleo kwa Manispaa ya Songea kwani umewezesha ujenzi wa stendi ya mabasi ya kisasa inayotarajia kuzinduliwa mwezi huu.
Naye Mhandisi wa mradi huo, Gilbert Mfinanga ambaye ndiye Msimamizi Msaidizi wa Mradi wa Uboreshaji Miji Tanzania (ULGSP), alisema mradi huo ulianza mwaka 2013 na unatarajia kumalizika mwaka 2018, utagharimu dola za Kimarekani milioni 255.
Washiriki wa mkutano huo ni pamoja na Wakurugenzi, Wahandisi, Wachumi, Maafisa Mazingira, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Watunza Hazina wa Halmashauri 18 pamoja na ujumbe kutoka nchini Uganda wakiongozwa na Waziri wa Nchi  Maendeleo ya Miji Bibi Rosemary Najemba. 

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa