Na
Lorietha Laurence-Maelezo
Jeshi la Polisi
nchini limetoa wito kwa wamiliki wa silahi
kujitokeza na kuhakiki silaha zao katika Wilaya wanazoishi kabla ya
kumalizika kwa zoezi hilo mnamo Juni 30 mwaka huu.
Hayo yalisemwa na
Msemaji wa Jeshi hilo Kamishna Msaidizi Advera Bulimba alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo jijini
Dar es Salaam.
“Serikali imetoa muda
wa miezi mitatu kukamilisha zoezi hili muhimu na tayari miezi miwili imepita
hivyo wale ambao bado hawajahakiki silaha zao kuzikakiki sasa kabla ya Juni 30
ili kuepukana na usumbufu” alisema Kamshna Msaidizi Bulimba na kuongeza kuwa:
“Natoa wito kwa watu
wote wanaomiliki silaha kinyume na sheria kusalimisha silaha hizo katika vituo
vya polisi, ofisi za serikali na kwenye nyumba za ibada na watakaofanya hivyo ndani ya muda ulipangwa
hawatachukuliwa hatua zozote za kisheria”.
Aliongeza kuwa baada
ya muda ulipangwa na Serikali kupita na wamiliki hawajahakiki silaha zao Jeshi
la Polisi nchini litaendesha operesheni
kali kuwakamata wale ambao hawakujitokeza
katika zoezi la uhakiki na hatua kali zitachukuliwa ikiwemo kufutiwa leseni na
silaha zao kutaifishwa na kuwa mali ya Serikali.
Aliwaomba ndugu wa
wale walikuwa wakimiliki silaha ambao wamefariki au ni wagonjwa wasalimishe
silaha hizo katika vituo vya Polisi kwa niaba ya ndugu zao ndani ya kipindi cha
uhakiki wa silaha.
Zoezi la uhakiki wa
silaha lilianza Machi 21 mwaka huu kufuatana na sheria ya usimamizi wa silaha na
risasi ya mwaka 2015, ambapo kifungu cha 66 cha sheria hiyo kinamtaka kila mmiliki
kuhakiki kumbukumbu za silaha yake au risasi
pale anapoamriwa na mamlaka.
Lengo la kuhakiki
kumbukumbu za wamiliki wa silaha ni kupata taarifa sahihi za wamiliki hao
zitakazosaidia kubaini wale wote wanaomiliki kinyume na sheria, kuwafahamu
wamiliki waliohama na kuhamia makazi mapya, kuwafahamu wamiliki waliofariki ili
kuzuia vitendo vya uhalifu na uvunjwaji wa amani nchini.
0 comments:
Post a Comment