Na Immaculate Makilika – MAELEZO , Tarehe 01.06.2016
Serikali ya
Tanzania yasifika kwa kuwa na uongozi unaozingatiaSheria na Utawala Bora.
Hayo yamesemwa
leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Angella Kairuki alipokuwa akifungua Mkutano wa siku
mbili wa Kimataifa kuhusu Utawala wa
Sheria na Utawala bora.
Lengo la mkutano
huo ilikuwa ni kujadili masuala ya
Afrika katika kukuza utawala wa sheria katika utekelezaji wa agenda ya
maendeleo endelevu ya mwaka 2030 na agenda ya Umoja wa Afrika ya 2063.
“Mkutano huu wa
kistoria nchini Tanzania utasaidia kuleta mageuzi katika Taasisi zinazosimamia
masuala ya Sera na Sheria ambayo yatachochea maendeleo mazuri katika nchi za
Afrika”, alisema Waziri Kairuki.
Akiendelea
kuzungumza Waziri Kairuki alisema uwepo wa Marais wastaafu kama Mhe.Benjamin
Mkapa na Dkt. Jakaya Kikwete, katika mkutano huo ni ushahidi tosha wakuwepo na
mafanikio ya utawala wa sheria na utawala bora nchini Tanzania.
Kwa upande wa
Rais Mstaafu Mhe.Benjamin Mkapa, amesema ili Bara la Afrika liendelee Kiuchumi
ni lazima watu wake wapate elimu ya uraia ili waweze kushiriki zaidi katika
masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo yao pamoja na kuwepo na uongozi
utakaoleta mabadiliko “transformative leadership”.
Naye, Waziri wa
Haki Sudani ya Kusini Mhe. Pwanauwilla Unango amesema pamoja na kuwa Bara la
Afrika lina matatizo mengi kama vita, njaa, magonjwa na ndoa za utotoni, dunia
isiitazame Afrika kwa mtazamo huo pekee, bali inahitaji msaada kutoka Jumuiya
za Kimataifa.
Mkutano huo
wenye kauli mbiu “Kufikia agenda ya 2030 na agenda ya 2063:Utawala wa Sheria
kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika”, (Achieving the 2030 agenda and agenda
2063:The rule of law as a driver of Africa’s suistainable development) ,
umeandaliwa na Shirika la Kimataifa la
Maendeleo ya Sheria (IDLO) la nchini Italia, kwa Ushirikiano wa Serikali ya
Tanzania umehusisha wadau mbalimbali
wakiwemo Mawaziri, kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mabalozi kutoka ndani na
nje ya Afrika pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya kutetea Haki za Binadamu.
Mwisho

0 comments:
Post a Comment