Frank Mvungi-Maelezo
Wakala wa Taifa wa Utafiti
wa Nyumba Bora na Vifaa vya Ujenzi (NHBRA) umeanza kufanya utafiti utakaosadia
kupunguza kiwango cha Hewa ya Ukaa (green house gases) kinachozalishwa kutokana na shughuli za ujenzi ili kupunguza uharibifu wa mazingira.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam Mhandisi Heri Hatibu kutoka wakala
huo amesema utafiti utasaidia kupunguza gharama za Ujenzi hapa nchini.
Akizungumzia Malengo
ya Utafiti huo Hatibu amesema kuwa, utasaidia kupunguza kiwango cha nishati
kinachotumiwa kwenye nyumba kwa ajili ya kupooza hewa hivyo kuokoa fedha
inayoweza kutumika kufanya mambo mengine.
“Sekta ya Ujenzi
inachangia asilimia 40 ya hewa ya ukaa hivyo lengo la utafiti huu ni kusaidia
kuondoa tatizo hili mara baada ya utafiti wetu kukamilika.” Alisisitiza
Mhandisi Hatibu.
Aidha Hatibu amesema
kuwa, utafiti huo utawezesha kusanifu majengo yatakayotumia nishati kidogo
kwenye hatua ya ujenzi na hata wakati wa matumizi ya majengo husika. Pia utachochea
matumizi ya vifaa vya Ujenzi vinavyopatikana katika maeneo ya karibu na shughuli
za ujenzi.
Pia utafiti huo
utasaidi kutoa elimu kwa wadau wa ujenzi kuhusu nishati mbadala katika
kutekeleza shughuli za ujenzi, ikiwemo kuacha kukata miti.
Vile vile wananchi
wataelimishwa kuhusu njia bora za uchomaji wa matofali ili waweze kutumia vifaa
vingine badala ya kukata miti kwa ajili ya uchomaji matofali.
Matokeo ya utafiti
huo unaotarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu yatasaidia wadau wa
sekta hii kupanga mipango ya ujenzi itakayosaidia kupunguza athari katika
mazingira zinazosababishwa na matumizi makubwa katika uzalishaji vifaa vya
ujenzi na hata katika ujenzi.Utafiti huo unafanyika katika Mikoa ya Dar es
salaam, Dodoma, Morogoro na Tanga.

0 comments:
Post a Comment