Kumekuwepo na taarifa mbalimbali zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii
zinazotokana na habari iliyoandikwa na kuchapishwa kwenye gazeti la Jambo leo
la tarehe 24 Juni, 2016, toleo namba 2482 yenye kichwa cha habari "Sasa ukimwi kupimwa nyumba kwa nyumba".
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kutoa ufafanuzi kwamba UKIMWI
HAUTAPIMWA NYUMBA KWA NYUMBA bali itafanya utafiti wa Viashiria na Matokeo ya
UKIMWI Tanzania kuanzia mwezi Septemba 2016 ambapo UKIMWI utapimwa kwenye kaya chache
ambazo zimechaguliwa kitaalam nchi nzima ili ziweze kuwakilisha kaya nyingine
nyingi ambazo hazitahusika moja kwa moja katika utafiti huu.
Utafiti huu utajumuisha kaya zipatazo 16,000 ambazo ni sampuli
iliyochaguliwa kisayansi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar na
utahusisha watu wazima wasiopungua 40,000 wakiwemo watoto takribani 8,000.
Aidha, katika utafiti huu kutakuwa na kupima homa ya ini, kupima wingi wa
chembechembe za damu yaani CD4, kupima wingi wa virusi katika damu
na kupima kiwango cha ufanisi wa dawa za kufubaza VVU kwa watu wanaotumia dawa
hizo.
Ifahamike kwamba, utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI wa mwaka
2016 unafanyika nchini kwa mara ya 4 ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka
2003, wa pili ulifanyika mwaka 2007 na wa tatu ulifanyika mwaka 2011.
Hivyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inapenda kuwatoa hofu wananchi kwakuwa utafiti
huu sio mpya katika nchi yetu na watanzania ambao wamekuwa wakipitiwa na
utafiti huu, wamekuwa wakitoa ushirikiano kwa zaidi ya asilimia 90.
Utafiti huu wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania utaendeshwa na Ofisi
ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara, Wizara ya Afya kwa Tanzania
Zanzibar, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Zanzibar (OCGS), Tume ya Taifa ya
Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) na Tume ya UKIMWI Zanzibar (ZAC).
Imetolewa na:
Mkurugenzi
Mkuu,
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),
Dar es Salaam,
28 Juni, 2016.
0 comments:
Post a Comment