Na: Veronica Kazimoto
Dar es Salaam.
UTUMIKISHWAJI
wa Watoto bado ni tatizo kubwa nchini ambapo kati ya watoto watatu
wenye umri wa miaka 5 - 17, mtoto mmoja anafanya kazi ambazo ni
hatarishi katika maisha yake kiafya, kimwili na kisaikolojia.
Hayo
yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge,
Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu Mhe. Dkt. Abdallah Possi
wakati wa uzinduzi wa Matokeo ya Utafiti wa Utumikishwaji wa Watoto
Tanzania wa Mwaka 2014 uliofanyika katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na
Mipango jijini Dar es Salaam.
Matokeo
ya Utafiti huo yameonyesha kuwa, kati ya watoto milioni 15 wenye umri
kati ya miaka 5 – 17, watoto milioni 4.2 sawa na asilimia 28.8
wanatumikishwa katika kazi mbalimbali za kiuchumi.
Matokeo
haya yameonesha kuwa hali ya utumikishwaji wa watoto umepungua kutoka
asilimia 31.1 kwa mwaka 2006 hadi asilimia 28.8 kwa mwaka 2014.
“Kutokana
na matokeo ya utafiti huu, ni dhahiri kwamba, utumikishwaji wa watoto
bado ni tatizo kubwa nchini na duniani kwa ujumla. Kwa mujibu wa takwimu
za Shirika la Kazi Duniani (ILO), asilimia 11 ya watoto wote duniani
sawa na watoto milioni 264 wenye umri wa miaka 5 – 17 wanatumikishwa
kwenye ajira za aina mbalimbali,” amesema Dkt. Possi.
Dkt.
Possi amesisitiza kuwa ni wajibu wa jamii kuwekeza katika elimu kwa
watoto kwa ajili ya kupunguza tatizo la utumikishwaji wa watoto ambao
unakwenda kinyume na haki zao.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina
Chuwa amesema utafiti huu umebainisha kuwa, watoto wanafanya kazi zaidi
katika sekta za Kilimo, Misitu na Uvuvi ambazo zinaajiri asilimia 92.1
ya watoto wote wanaojishughulisha na shughuli za kiuchumi.
Dkt.
Chuwa ameongeza kuwa watoto hutumia zaidi ya nusu ya muda wao sawa na
asilimia 58.8 kwa siku nzima kujihudumia na kufanya usafi binafsi ambapo
wasichana wameonekana kutumia asilimia 59.2 na wavulana hutumia
asilimia 58.3 kujihudumia.
Aidha,
shughuli za kujisomea kwa watoto ni asilimia 15.5 ambapo wavulana
wanatumia muda mrefu zaidi kujisomea kwa asilimia 16.4 na wasichana
hutumia asilimia 14.6 kujisomea.
Utafiti
huu umebainisha viashiria vya hali ya watoto wanaofanya kazi za
kiuchumi na zisizo za kiuchumi, hali ya utumikishwaji wa watoto pamoja
na athari mbalimbali ambazo watoto wanapata kwa kujihusisha na shughuli
mbalimbali za kiuchumi.
Matokeo
yameonesha pia, utumikishwaji ni mkubwa kwa watoto wasiosoma
ikilinganishwa na watoto wanaosoma. Aidha, matokeo yameonesha
utumishwaji ni mkubwa katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo
ya mjini.
Utafiti
huu wa Utumikishwaji wa watoto wa mwaka 2014 ni wa tatu kufanyika
nchini ambapo utafiti wa kwanza ulifanyika mwaka 2001 na wa pili
ulifanyika mwaka 2006.
0 comments:
Post a Comment