Na. MWANDISHI WETU
Shirika
la Umoja wa Mataifa la Upunguzaji Athari za Maafa (UNISDR) kwa
kushirikiana na Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu
wameendesha mafunzo ya siku mbili kwa wadau wa masuala ya maafa juu ya
namna ya kutumia Kanzi Data ya takwimu za Athari za Maafa kutoka Wizara
na Taasisi za Serikali nchini.
Mafunzo
hayo yalifanyika Julai 19 na 20, mwaka huu katika Ofisi ya Waziri Mkuu
na kushirikisha Wizara na Taasisi za Serikali ikiwemo; Wizara ya Maji na
Umwagiliaji, Wizara ya Ulinzi na Usalama wa Taifa, Wizara ya Kilimo,
Chakula na Ushirika, Jeshi la Zima Moto, Jeshi la Polisi, Mamlaka ya
Hali ya Hewa, Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu, TAMISEMI, Chuo
Kikuu cha Ardhi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Ofisi ya Taifa ya
Takwimu.
Mafunzo
hayo yalijikita katika kusaidia wadau wa masuala ya maafa katika
kuongeza uwezo wa kuwa na Takwimu sahihi za majanga yanayoikabili Nchi
ya Tanzania.
Akizungumza
wakati wa Mafunzo hayo Mratibu wa Masuala ya Maafa Shirika la Umoja wa
Mataifa la Upunguzaji Athari za Maafa, Bw. Adam Fysh alieleza kuwa,
Mafunzo hayo yatasaidia kuongeza uboreshaji wa kumbukumbu za maafa
nchini, “kama ilivyokusudiwa, mafunzo yatasaidia kuwa na rekodi za
kutosha, yatasaidia ufuatiliaji, kuwa na tathimini za mara kwa mara, na
ulinganifu wa kujua nchi zingine zinafanya nini katika kukabiliaana
na athari za maafa, mafunzo haya pia yatasaidia wahusika kufanya maamuzi
sahihi na kwa wakati katika maendeleo hususani kwa kupunguza athari za
maafa hapa nchini”
Bw.
Fysh aliongeza kuwa kiu yake ni kuona nchi zinajikita katika utoaji wa
taarifa zenye uhalisia na sahihi ili kuwa na kumbukumbu na takwimu zenye
kusaidia Dunia kujua maafa yanayotokea, “Natamani kuona tunakuwa na
takwimu sahihi na zenye mpangilio zinazohusu athari za maafa hususani
yanayoikabili nchi’
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idaya ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig. Jenerali, Mbazi Msuya alishukuru
jitihada za Shirika hilo kwa kuona umuhimu wa kuwajengea uwezo wadau wa
masuala ya Maafa na kueleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati na
yataleta manufaa makubwa kwa Taifa.
“Nawapongeza
Shirika kwa kuona ni vyema kuifikia Tanzania kwa kuijengea uwezo wa
namna ya kuweka taarifa muhumu za masuala ya Maafa katika kanzi
data. Hii itatusaidia sana katika kupanga mipango yetu kwa namna bora
zaidi na vile vile itarahisha katika kufuatilia kufanya tathmini”,
Alisema Brig. Msuya
Naye
Mtaalam wa Masuala ya Hali ya Hewa kutoka Mamlaka ya Hali ya
Hewa, Bi.Hellen Msemo alieleza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kutoa fursa
za kimaendeleo kwakuwa takwimu za athari za maafa zitasaidia kuwa na
mipango mizuri ya maendeleo ya nchi na kuipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu
kwa kuona umuhimu wa kuratibu mafunzo hayo.
Mafunzo
ya kutumia Kanzi Data ya takwimu za Athari za Maafa tayari yamezifikia
nchi 31 duniani huku Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi kumi na tatu za
Afrika zilizonufaika na elimu hiyo.
0 comments:
Post a Comment