Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO
Chama
cha Waigizaji cha Mkoa wa Kinondoni (STDFAA) wamemuomba Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Nape Nnauye kuiharakisha Sera
ya filamu ili iwasaidie katika mambo mbalimbali hususani ya kisheria.
Hayo
yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu wa Chama hicho, Jafari
Makatu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa
pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na kuzungumzia changamoto
zinazowakabili katika tasnia ya filamu nchini.
Makatu
amesema kuwa Sheria ya Filamu ni muhimu katika tasnia hiyo hivyo
ikiharakishwa itasaidia wadau wa tasnia hiyo kufanya kazi kwa uwazi na
usalama wa hali ya juu kwa kuwa watakua wanalindwa na sheria.
“Tunamuomba
Waziri wetu Mhe. Nape atuharakishie Sera ya Filamu kwa sababu sheria
hiyo itatusaidia kuoanisha mambo mbalimbali ya kisheria kuanzia kwenye
uandaaji wa kazi zetu hivyo, kupelekea kufanya kazi kwa ufanisi na kutoa kazi bora zaidi”. Alisema Makatu.
Ameongeza
kuwa sheria hiyo pia itawasaidia katika suala zima la Haki miliki na
Haki shiriki, malipo stahiki kwa kila kazi, masoko, madaraja ya
waigizaji na wadau wote wa tasnia ya filamu pamoja na ulazima wa kila
msanii kujiunga katika vyama husika vitakavyowasaidia katika mambo
mbalimbali.
Aidha,
Katibu huyo ameiomba Serikali kuwekeza kwenye sanaa ili kuwawezesha
kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi na kuchangia katika Pato la Taifa pia
amemuomba Mhe.Nape kuwatafutia eneo maalum la ardhi ambalo litawasaidia
katika kufanyia shuhuli zao za kurekodi filamu.
Ametoa
rai kwa wasanii kujiunga katika vyama mbalimbali vinavyowahusu ili
kuleta umoja, mshikamano na tija katika kazi za sanaa,amesisitiza
wasanii kujiunga na Bima za Afya.
Naye
Mdhamini wa Chama hicho, Ahmed Olotu amewaomba waandishi wa habari
kutumia kalamu zao katika kuwasaidia wasanii kupambana na wauzaji wa
filamu feki kwa kuwa wanarudisha nyuma maendeleo ya wasanii na kupunguza pato la Taifa.
0 comments:
Post a Comment