Hussein Makame na Abushehe Nondo-MAELEZO
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Bashiru Ally amesema hakuna udikteta kwenye utawala wa awamu ya tano wa
Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Dkt. Bashiru alisema hayo
katika mahojiano Maalum na Idara ya Habari-MAELEZO ofisini kwake jijini Dar es
Salaam hivi karibuni, kuhusu nidhamu na uadilifu Serikalini.
Kauli hiyo ya Dkt. Bashiru
inakanusha madai ya baadhi ya wanasiasa kuwa Serikali ya sasa ni ya kidikteta na kueleza kuwa Serikali ya Rais
Magufuli ni yenye nidhamu na uadilifu kwa wananchi inaowatumikia.
Alisema lugha ya udikteta
inayozungumzwa na baadhi ya watu inaashiria kuwa Watanzania hawajaafikiana juu
ya namna ya kusimamiana ili anayetenda kwa nidhamu na uadilifu atukuzwe na
asiyetenda kwa nidhamu na uadilifu aadhibiwe kwa mujibu wa sheria.
“Hata
hii lugha inaitwa ya udikteta, mimi nikiisikiliza naona kuna kutofautiana sana
tangu Rais Magufuli ameingia madarakani, juu ya namna ya kusimamiana ili wanaotimiza wajibu wao wasifiwe, watukuzwe watunukiwe
na wale wasiotimiza kwa maana wanaotuangusha waadhibiwe kwa
misingi na taratibu zilizowekwa”, alisema Dkt Bashiri na kukelezea upotoshwaji kuwa:
“Kuna mjadala hata kama si wa
kitaifa au mkubwa, lakini ukifuatilia kwenye vijiwe na kwenye vyombo vya habari
unaona tunatofautiana sana katika uelewa juu ya nidhamu na uadilifu, na mimi
silaumu hao wanaokwenda mbali na kusema huu sio usimamizi mzuri, bali ni
udikteta.
“Mimi sikubaliani nao lakini
wanatusaidia kutuambia bado tuna tatizo la kutokukubaliana na kwamba hatuna
ufahamu wa pamoja juu ya hicho tunachokiita nidhamu na uadhilifu kazini.”
Alifafanua
kuwa Rais Magufuli bado yupo sahihi katika uongozi wake na watanzania wamempa
mamlaka ya kuongoza, hivyo ni lazima kuheshimu uongozi uliopewa dhamana na
wananchi , badala ya kumkwamisha, kumdharau na kumbeza kwani yeye ndiye
anayebeba mamlaka hiyo.
Dkt.
Bashiru alisema hakuna mjadala na ni dhahiri kwamba mkakati wa Rais
Magufuli kwa miezi tisa aliyokaa
madarakani, unajenga upya nidhamu na maadili au uadilifu hasa katika utumishi
wa umma” alisema Dkt. Bashiru na kuongeza:
“Mjadala uliopo ni jinsi
gani mkakati huo unatekelezwa, wapo wanaotamani Rais aongeze kasi mara mbili na wanadhani wale
wanaomkosoa wanamchelewesha katika azma yake ya kutimiza ahadi alizowaahidi Watanzania”
alisema Dkt. Bashiru na kuongeza:
“Na wengine wanadhani
abadilishe mkakati.Sasa itatuchukua muda kuja kupima lakini kwa mtu
anayefuatilia miezi tisa inatosha kuonesha muelekeo, bado yupo katika muelekeo sahihi.”
Akizungumzia siasa na
wanasiasa, Dkt. Bashiru alisema anachelea kusema kuwa kwenye siasa kumeingia
ubabaishaji kwani haridhiki na utendaji wa baadhi ya viongozi wa kisiasa.
“Mimi sitaki kusema kwamba kwenye siasa
kumeingia ubabaishaji nitaonekana labda sina nidhamu, lakini siridhiki kwa
namna viongozi wetu wa kisiasa, yaani sijaridhika na utendaji wao” alibainisha
Dkt. Bashiru na kufafanua kuwa:
“Siridhiki kwa namna wanavyosimamia majukumu yao kwenye taasisi zao, wengi wao wanatumia nafasi
zao za uongozi, utendaji kazi wao na kauli zao kuwatenganisha wananchi na Serikali
yao, badala ya kuwaunganisha kwa pamoja.
“Na hapa asiwe anatajwa Rais
peke yake kanakwamba yeye ndiye ameomba kura peke yake, bali kuna maelfu ya
watu wameomba kura katika nchi hii na kupewa dhamana , hivyo watapimwa
wamefanya nini katika nafasi zao miaka mitano ijayo.Wanasiasa wetu na utendaji
wao na kauli zao hasa katika kuwatenganisha wananchi ”.
Akitoa ushauri Dkt Bashiru
aliwataka wanasiasa, wasomi na vyombo vya habari wasiisaliti nchi yao badala
yake watekeleza wajibu wao kwa umma ili warejesha nidhamu na uadilifu
uliokosekana nchini ambazo ni tunu zilizoachwa na waasisi wa Taifa la Tanzania.
“Kwa sababu maeneo mengi ya
tatizo hili tunalolisema, wahusika wakubwa ni sisi.Haingii kilaza mahakamani
akawa jaji, ni mtu aliyesoma, huwi wakili, mwandishi wa habari mpaka umesoma na
sasa hivi kuna muelekeo huo huwi mwanasiasa mpaka umesoma” alisema Dkt.
Bashiru.
Alisema uwekezaji mkubwa wa
Serikali katika elimu umewezesha kupata wasomi katika kila ngazi, kwa hiyo ni
vyema wakatekeleza wajibu wao kwa nidhamu na uadilifu ili kusitokee makosa kama
ya watumishi hewa na majipu.
“Mwalimu Nyerere alisema
msomi akishapata neema ya kusomeshwa alafu asiwajibike kwa waliomsomesha, huo
ni usaliti” alisema Dkt. Bashiru.
Dkt. Bashiru aliwataka
wasomi wa kada mbalimbali kurekebishana pale wanapokiuka maadili ya taaluma
zao, badala ya kusubiri kulalamika pale maamuzi yanapochukuliwa dhidi yao kwani
hayo ni matokeo ya vyama vya kitaaluma kutotimiza wajibu wao.
Alisema iwapo mawakili,
walimu, madaktari wakiisimamiwa vyema na vyama vyao vya kitaaluma, nidhamu na
uadilifu vitarejea nchini na hivyo kufanikisha utekelezji wa mipango ya
maendeleo ya nchi.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment