Na Jonas Kamaleki, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt.
John Pombe Magufuli ameagiza waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota kukaa
kwenye nyumba za Serikali miaka mitano bure na baadaye kuzinunua kwa bei
nafuu.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es
Salaam wakati akiwahutubia wakazi wa Magomeni na kuagiza ujenzi wa
nyumba hizo kuanza ndani ya miezi miwili.
“Nasema wakandarasi ndani ya miezi miwili waanze
kujenga nyumba 644 kwa ajili ya wazee ambao wameteseka sana baada ya
nyumba zao kuvunjwa, nitatoa fedha Serikalini mwezi huu kwa ajili ya
kuanza kwa shughuli hiyo” alisema Dkt. Magufuli.
Ameongeza kusema kuwa ujenzi huu anataka
ukamilike ndani ya mwaka mmoja au miezi sita kama ulivyokuwa kwa hosteli
za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema atafurahi kukabidhi hati kwa wakazi wa Magomeni Kota pindi nyumba hizo zitakapokuwa zimekamilika.
“Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uzima ili nyumba hizo zikiwa tayari hati nizikabidhi mwenyewe,”alisema Magufuli.
Rais Magufuli ameonyesha kukerwa na vitendo vya
baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waaminifu kuwanyima haki wanyonge.
Amesema vitendo hivyo vya unyanyasaji viishe mara moja na watanzania
wakae kwenye nchi yao kwa amani.
Aidha, Rais Magufuli amemwagiza Mkurugenzi Mkuu
wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu kukusanya madeni
yote ya kodi kwa wanaodaiwa na shirika hilo bila kujali chama, serikali
au mtu yeyote
.
Ameagiza kuwa wanaodaiwa inabidi walipe deni lao ndani ya siku 7 (saba) vinginevyo waondolewe kwenye nyumba hizo.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi amemshukuru Rais Magufuli kwa
kuwajali wanyonge hasa kwa kutatua mgogoro wa makazi kwa wakazi wa
Magomeni Kota.
“Mheshimiwa Rais ninakushukuru kwa kuwajali wazee
hawa wa Magomeni, nami nilitekeleza maagizo yako na kufuatilia mgogoro
huu hadi kupata ufumbuzi”, alisema Lukuvi.
Lukuvi amesema kuwa mgogoro wa Magomeni
ulivyokuwa mkubwa ulistahili nguvu ya Mhe. Rais Magufuli, lakini kwa
migogoro mingine ambayo ni midogo, hiyo ameishughulikia na ataendelea
kuishughulikia ili kero za wananchi kuhusu ardhi ziishe kama
alivyoagizwa na Rais.
Nyumba zilizokuwa Magomeni Kota zilivunjwa mwaka
2009 na wananchi wakaahidiwa kujengewa nyumba ambazo wangeuziwa kwa bei
nafuu. Lakini kwa takribani miaka mitano nyumba hizo hazikujengwa hali
ambayo iliwafanya wakazi hao waishi maisha ya kuangaika.
Hivi karibuni Mhe. Rais John Pombe Magufuli
alifuta hati zote za umiliki eneo la Magomeni Kota na kuondoa usimamizi
wa Nyumba TAMISEMI na kuupeleka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kwa ajili ya kuanza kusimamia ujenzi.
0 comments:
Post a Comment