Na Anitha Jonas – WHUSM
DAR ES SALAAM.
Heko
Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo kwa kusimamia ujenzi wa
mageti ya kielektroniki katika kuboresha makusanyo yatokanayo na michezo
iinayofanyika Uwanja wa Taifa.
Hizo
ni pongezi zilizokuwa zikitolewa kwa uongozi wa Wizara kutoka kwa wadau
wa michezo hivi karibuni mara baada ya kuzinduliwa kwa mfumo wa kisasa
wa mageti ya kieletroniki ambayo hutumia kadi maalumu ambazo ndiyo
huruhusu mageti kufunguka na mtu kupita.Hivyo basi namna hiyo ya mageti
hayo yanavyofanya kazi ndiyo huleta tafsiri ya mfumo wa mageti ya
kieletroniki.
Akizungumza
katika makabidhiano ya mageti hayo ya kieletroniki yaliyoko katika
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo, Mhe.Nape Moses Nnauye alisema kwa kufanikisha hilo kumeifanya
Tanzania kuwa nchi ya kwanza kuwa na mageti ya kisasa katika ukanda
huu wa Afrika Mashariki. Na hii ni sehemu nzuri.
Kukamilika
kwa ujenzi wa mageti hayo kunafuatiwa na agizo la Waziri Mkuu
Mhe.Kassim Majaliwa alipofanya ziara ya kikazi uwanjani hapo mnamo
Februari 17,2016 na kumwagiza Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na
Michezo kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa haraka kwa kuwa ni
sehemu ya mkataba wa ujenzi wa uwanja.
Pamoja
na hayo Waziri Nnauye alieleza kuwa mfumo huo umeandaliwa na Kampuni ya
kizalendo ya SELCOM Tanzania ambapo hao ndiyo watakao kuwa wasambazaji
wa Kadi hizo kwa nchi nzima na kadi hizo zitakuwa zikipatikana kwa
mawakala wao wote na zitatolewa bure pasipo kugharamia kiasi chochote
cha fedha bali kitakacho hitajika ni kuzijaza kadi hizo fedha.
“Kwa
niaba ya Waziri Mkuu napenda kuwasilisha pongezi zake kubwa kwa Kampuni
ya China ya BCEG kwa kukamilisha mradi huu wa mageti ya kisasa kama
ilivyokuwa sehemu ya ujenzi wa uwanja mbali na kupitia changamoto
mbalimbali,pongezi nyingi pia kwa Kampuni ya SELCOM kuifanya kazi hii
kwa uaminifu mkubwa,”alisema Waziri Nape.
Kwa
upande wa namna ya matumizi ya kadi hizo mdau yeyote wa mpira
atahitajika kusajili kadi yake kwa kutoa taarifa zake binafsi za muhimu
ikiwa ni pamoja na namba yake simu ambapo taarifa hizo zitahifadhiwa na
na itakapotokea kadi yako imechukuliwa na mtu mwingine yoyote na
kufanya malipo yoyote ujumbe utaingia kwenye simu yako kukutaarifu kuwa
kadi yako inafanya malipo na hii ni kwa sababu kadi hizi zina uwezo wa
kutumika kwa vitu mbalimbali ikiwemo kulipa bili za maji,kununua
LUKU,kununulia mafuta katika vituo mbalimbali pamoja na kununulia vocha.
Pia
mara baada ya kufika uwanjani hapo kitakachohitajika kwa mtu yeyote
atakayefika uwanjani kwa lengo la kuingia kushuhudia mechi ni kuweka
kadi yake kadi kifaa maalum kilichopo katika mageti hayo ambacho ndicho
kinachofungua na kufunga mageti hayo.
Pamoja
na hayo ilielezwa kuwa kila mdau wa michezo inayofanyika uwanjani hapo
atakuwa na uwezo wa kukata tiketi kupitia kadi yake kulingana na uwezo
wake na atachagua ni sehemu gani ya viti atakapoketi kulingana na tiketi
aliyokata kama ni VIP au viti vya Bluu au Rangi ya Chungwa (Orange)
kutakuwepo na mashine maalum za kutambua ni wapi utaketi kulingana na
tiketi yako.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo
Prof.Elisante Ole Gabriel aliwatoa hofu watanzania katika sherehe za
makabidhiano ya mageti hayo kwa kusema kadi hizo zitaweza kumilikiwa na kila mtu na siyo kwa watu maalum tu kwani kadi hiyo ndiyo itakayompa mtu yeyote uwezo wa kuingia uwanjani hapo.
Mfumo
huu utakuwa na faida zifuatazo mbali mbali kama Kuboresha mfumo wa
ukusanyaji wa mapato ya mechi zinazofanyika uwanjani hapo tofauti na
ilivyokuwa awali ambapo kulikuwepo na wizi wa tiketi ambao ulichangia
kwa kiasi kikubwa kuzorotesha zoezi la ukusanyaji wa mapato kwani kwa
sasa pale mtu anapokata tiketi tu pesa hiyo inaigia moja kwa moja na
kufanyiwa mgao kupitia mtandao bila kujali mtu huyo atahudhuria mechi
hiyo au la.
Faida
nyingine ni kuimarisha usalama zaidi kwani awali pesa zilizokuwa
zikikusanywa kwa makato ya tiketi zilikuwa zikihitaji ulinzi mkubwa
katika kuzihesabu na kuzihifadhi na kuzigawa kwa wadau wanaonufaika na
mgao wa mapato yatokanayo na mechi, pamoja na taarifa za watu watu wote
watakaoingia uwanjani zitakuwa zimehifadhiwa katika mfumo.
Vile
vile matumizi ya yatarahisisha kupunguza foleni na kuweza kupitisha
watu wengi zaidi kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali. Hivyo
itapunguza kero kwa mashabiki wanaofika uwanjani hapo kutizama mechi
kukaa muda mrefu katika mistari ya kuingia uwanjani.Hakika kutumika kwa
mfumo huu kutasaidia kuendeleza huduma za michezo nchini na kufikia
kiwango cha Kimataifa .
Katika
mazungumzo ya moja kwa moja na Meneja Mradi wa Ujenzi wa Mageti hayo
kutoka SELCOM Bw.Gallus Runyeta alitoa wito kwa watanzania kufika kwa
mawakala wao kwa ajili ya kujipatia kadi hizo mapema kabla ya kufufikia
siku za mechi ili kuondoa usumbufu wowote ambao ungeweza kujitokeza.Pia
alieleza kuwa kadi hizo zinatarajiwa kuanza kutumika kwa majaribio
katika mechi ya Simba na Yanga itakayofanyika uwanjani hapo Oktoba Mosi
mwaka huu.
Naye
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchi Bw.Jamal Malinzi aliipongeza
serikali kwa kuanzisha mfumo huo wa kisasa wa kukusanya mapato kwani
utasaidia kupunguza kelele za mgao tofauti na awali na pia aliiomba
serikali kuhakikisha mgao huo unawafikia wadau husika kwa wakati kwani
vilabu huhitaji pesa hizo kwa haraka sababu ndiyo wanazozitegemiea
katika uendeshaji wa shughuli zao.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya BCEG nchini Bw. Cheng Long Hai ambayo
ndiyo kampuni iliyojenga uwanja huo aliishukuru serikali kwa kuipa
ushirikiano katika kipindi cha ujenzi wa uwanja huo na kuahidi kusimamia
vyema matumizi ya mageti hayo kwa kipindi cha mwaka kama walivyotiliana
saini katika mkataba na serikali.
Pia
alisema kuwa anajivunia kwa kiasi kukubwa kujenga uwanja huo ambao
ameweza kukamilisha kama mkataba ulivyokuwa unasema na hii ni faraja
kwake kuweza kutimiza kila ilichohitajika kulingana na uhitaji na
aliendelea kusema kuwa kuwepo kwa mageti hayo ya kisasa katika uwanja
huo kunaufanya uzidi kuoneka wa kisasa zaidi barani Afrika na kwa Kanda
ya Afrika Mashariki.
Naye
mmoja wa wadau wa soka nchini Bw. Hussein Makame mkazi wa Magomeni
jijini Dar es Salaam alitoa maoni yake kwa kuuomba uongozi wa SELCOM
kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kutumia kadi hizo kabla ya siku za
mechi kwa uwezo wa uelewa wa kila mtuaingiea uwanjani pale ni tofauti na
kwa kufanya hivyo watapunguza usumbufu.
Pamoja
na hayo, Bw. Hassan Silayo, mkazi wa Kimara Suka jijini Dar es Salaam
ambaye nae ni mkereketwa wa soka la nchini aliishauri serikali kuweka
ulinzi wa kutosha katika mageti hayo kwa siku ya kwanza kutakapokuwa na
mechi kwa lengo la kulinda waharibifu wa miundombinu hiyo; kwani
kumekuwa na kawaida ya baadhi ya mashabiki wanapofungwa kuharibu
miundombinu pia alitoa pongezi nyingi kwa serikali kwa kuleta maendeleo
kama hayo katika sekta ya michezo.
Hata
hivyo mpaka sasa SELCOM wameshatoa kadi za viongozi wakuu nchini za
kuingilia katika mageti ya uwanja huo akiwemo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais na
Waziri Mkuu ambapo kadi zao alikabidhiwa Waziri wa Habari wa Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe.Nape Moses Nnauye kwa ajili ya kuwapatia viongozi
hao katika sherehe za makabidhiano ya mageti hayo kwa serikali.
0 comments:
Post a Comment