Home » » Naibu Waziri wa Habari kuwa mgeni rasmi Tamasha la Sanaa

Naibu Waziri wa Habari kuwa mgeni rasmi Tamasha la Sanaa

 
Na Beatrice Lyimo

Maelezo

Dar es Salaam.
22/09/2016

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Annastazia Wambura anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tamasha la Sanaa litakalofanyika  Septemba 24, mwaka huu katika kijiji cha Makumbusho Jijini Dar salaam.

Tamasha hilo ni sehemu ya maandalizi ya matamasha yanayofanyika katika kuelekea maadhimisho ya kilele cha Siku ya Msanii Tanzania inayotarajiwa kufanyika Octoba 29 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Haak Neel Production Bw. Godfrey Mahendeka alisema kuwa lengo la tamasha hilo ni kutambua, kuhamasisha na kuthamini kazi na machango unaotolewa na wasanii nchini.

Amesema kuwa Tamasha hilo litawakutanisha wasanii wa aina zote ikiwemo Sanaa za muziki, filamu, ufundi na maonyesho ili kuonyesha umahiri wao kwa hadhira.

“Kwa mara ya kwanza tamasha hili linawakutanisha wasanii aina zote kwenye eneo moja yaani sanaa za muziki, filamu, ufundi na maonyesho ili kuonyesha umahiri wao kwa hadhira” alifafanua Bw. Mahendeka.

Aidha, aliongeza kuwa tamasha hilo litapambwa na shughuli mbalimbali ikiwemo huduma ya uchangiaji damu, elimu ya mifuko ya jamii kwa wasanii na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake mwakilishi kutoka Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) Bw. Augustino Makame aliwataka wasanii wa fani zote kujitokeza kwa wingi kwani siku hiyo ni fusra ya wasanii hao kubadilishana mawazo na uzoefu walionao.

Naye Msanii wa Bongo Fleva na mmoja wa wasanii watakaoshiriki tamasha hilo Bw. Peter Msechu ameipongeza Serikali kwa kuwajali wasanii na kupelekea kuundwa kwa idara itakayoshughulikia masuala ya sanaa.

Hata hivyo, Msanii huyo ametoa wito kwa Serikali kuzidi kufuatilia kazi za wasanii na kuzuia kuingiza kazi za wasanii ambazo hazijajkidhi vigezo zinazotoka nje ya nchi.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa