Home » » PROF. MBARAWA: WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI WASIO NA NIDHAMU WACHULIWE HATUA ZA KISHERIA.

PROF. MBARAWA: WABUNIFU MAJENGO NA WAKADIRIAJI MAJENZI WASIO NA NIDHAMU WACHULIWE HATUA ZA KISHERIA.




Na Abushehe Nondo
MAELEZO
Dar es Salaam
22.9.2016

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameiagiza bodi ya usajili wa wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi kuwachukulia hatua za kali za kinidhamu wakadiriaji majengo ambao sio waadilifu na waaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Prof Mbarawa aliyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua semina ya 26 ya siku moja  iliyowashirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya Ujenzi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere.

Waziri Mbarawa alisema kuwa wasanifu majengo na wakadiriaji wa majenzi ambao sio waaminifu katika taaluma yao wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali ili za kinidhamu ili fundisho kwa wengine.

“Wale wote ambao wanaleta ujanja ujanja katika taaluma hii ya usanifu majengo na ukadiriaji majenzi naagiza wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kutangazwa kwenye vyombo vya habari ili kila mtu ajue kama sio waadilifu” alisema Prof Mbarawa.

Alisema taaluma hiyo ni muhimu sana katika sekta ya ujenzi hivyo inapaswa kuheshimiwa kama zilivyo taaluma nyingine hivyo watakaokwenda kinyume na matakwa ya taaluma hiyo ni bora wakae pembeni kupisha wale wenye weledi.

Prof Mbarawa alisema  kuwa Serikali bado ina imani na wasajili majengo  na wakadiriaji majenzi wa ndani na kuwataka kuchangamkia fursa mbalimbali za kazi zinazotangazwa na Serikali.

Alisema hivi karibuni Serikali itaanza ujenzi wa reli ya kati sambamba na ujenzi wa baadhi ya viwanja vya ndege katika mikoa hivyo kuwataka kuungana kuwa kitu kimoja ili iwe rahisi kwao kupata kazi katika miradi hiyo.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Usajili wa wabunifu wa majengo na wakadiriaji majenzi Jehad Jehad alisema kuwa semina hiyo ina lengo la kuwanoa wabunifu majengo na wakadiriaji wa majenzi katika sekta ya ujenzi ili kutambua fursa ambazo zipo katika soko la Afrika Mashariki (EAC) na lile la nchi za jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa Afrika (SADC).

Jehad pia aliwataka wadau wa sekta ya ujenzi kutambua umuhimu na faida ya sheria ya mitandao katika kuboresha huduma zao kwa wananchi pamoja na kubadilishana  uzoefu wa kazi zao za kitaaluma kwa lengo la kuongeza weledi.

0 comments:

 
Supported byBlogs za Mikoa
Copyright © 2012. Dar es salaam Yetu - All Rights Reserved
Designed by Blogs za Mikoa
Proudly powered by Blogs za Mikoa