Na Sheila Simba, MAELEZO
Jumla ya shilingi bilioni 1.4 zimechangwa na mabalozi na
wafanyabiashara kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea
Mkoani Kagera.
Michango hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam katika
harambee iliyoongozwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa na
kufanyika Ikulu.
Akizungumza katika harambee hiyo Waziri Mkuu alisema jumla
ya nyumba 840 zimebomoka na kuharibika kabisa, wakati nyumba 1264 zimepata
hitilafu na zinaweza kufanyiwa marekebisho ili watu waendelee kuishi katika
nyumba hizo.
Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa shule 4 za sekondari ambazo ni
Nyakato, Ihungo, Kashange na Buhembe zimeharibika na mbili kati ya hizo yaani
Ihungo na Nyakato zimefungwa kutokana na
kuharibika sana.
Madhara mengine yaliyosababishwa na tetemeko hilo kwa mujibu
wa Waziri Mkuu ni kuharibika kwa vituo vya afya, miundombinu ya barabara, umeme
na njia za mawasiliano na kufanya athari za tetemeko kuwa kubwa.
Kutokana na athari hizo Waziri Mkuu amewaomba mabalozi
wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini kusaidia waathirika kwani ni tukio ambalo
halikutarajiwa na limeleta hasara kubwa kwa wanakagera na Taifa kwa ujumla.
“Licha ya michango hii ninayowaomba leo, tutaandaa safari
kwa anayehitaji kwenda kujionea hali halisi ili aone ni namna gani
atakavyosaidia,”alisema Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Majaliwa amesema kuwa imefunguliwa akaunti ya
kuchangia katika maafa hayo kwenye benki ya CRDB inayojulikana kama KAMATI
MAAFA KAGERA akaunti namba 0152225617300 na swift code ambayo ni CORUtztz na
kuwaomba wananchi na watu wengine kutumia akaunti hiyo kwa kusudi hilo.
Majaliwa amesema pia kuwa utaratibu unaandaliwa ili
kuwawezesha watu kuchangia kwa njia ya Mpesa, tigopesa na Airtelmoney.
Utaratibu huo utakapokuwa tayari utatangazwa ili kuwarahisishia watumiaji wa
mitandao hiyo kuchangia.
Katika harambee hiyo wafanyabiashara waliochangia ni
Mwenyeki Mtendaji wa kampuni za IPP Dkt Reginald Mengi aliyechangia Tsh million
110, Mohamed Dewji ametoa milioni 100, Subash Patel milioni 150 na Salim Turki
aliyetoa mifuko 5000 ya saruji na mabati
3000.
Wengine waliochangia ni kampuni mbali mbali zikiwemo kampuni
ya bia ya Serengeti iliyotoa mifuko 800 ya saruji, Sahara Tanzania wametoa
shilingi milioni 20, Camel Oil kupitia Camel Cement wametoa mifuko 1000 ya
saruji ,Puma wamechangia shilingi million 50, Pepsi Cola wametoa milioni 50 na
Azania Group wamechangia milioni 50.
Baadhi ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini
waliochangia ni pamoja na ubalozi wa China shilingi milioni 100 na kupeleka
madaktari,dawa,mahema na vifaa vingine kwa ajili ya kusaidia waliopatwa na
maafa hayo.
Kuwait kupita ubalozi wao nchini wamechangi dola elfu 10 za Kimarekani
na euro elfu 10, na Nchi ya Kenya
iliyopeleka msaada wa mahema,magodoro na dawa.
Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki
wametoa milioni 10, mwakilishi wa China Merchantile Group ametoa milioni 100,
Toyota Tanzania milioni 10, Kamal Group milioni 50, Urban Group milioni 20, TBL
milioni 100, IPTL 50, Tanzania Agriculturak Processing Zone milioni 30, Umoja
wa wafanya biashara ya mafuta ya rejereja milioni 250 na Group Six wametoa tani
80 za saruji.
Wengine waliochangia ni pamoja Jambo plastic milioni 20,
Tanga Cement mifuko 1000 ya saruji, Agusta Tz milioni 10, Oryx milioni 50,
Kagera Sugar milioni 100 na tani 10 za sukari, Tipper milioni 20 ambapo GBP,
Oilcom na Moil watajenga shule mbili zilizoharibika.
Uchangiaji huo umejumuisha pia na watu binafsi ambao ni wakili
wa kujitegemea, Bwana Protase Ishengoma milioni 5 na Melisa Kataraiya milioni
20.
Tetemeko hilo la ardhi ni kubwa kuliko yote ambayo yamewahi
kutokea hapa nchini na hadi sasa limesababisha vifo vya watu 17 na kuharibu
nyumba, majengo na miundombinu mkoani Kagera.
0 comments:
Post a Comment