RAIS John Magufuli ameteua wabunge wawili wapya wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania akiw2mo msomi maarufu nchini, Profesa
Palamagamba Kabudi na Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu jana
kwa vyombo vya habari, pia Rais Magufuli amemteua Benedicto Martin
Mashiba kuwa Balozi.
“Wabunge wateule hawa wataapishwa kwa taratibu za Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania,” ilieleza taarifa ya Ikulu na kuongeza kuwa kituo
cha kazi na tarehe ya kuapishwa kwa Balozi mteule Mashiba itatangazwa
baadaye.
Uteuzi wa wabunge hao wawili, Profesa Kabudi na Bulembo unafanya Rais
Magufuli afikishe idadi ya wabunge wanane kati ya 10 ambao kikatiba
anaruhusiwa kuwateua.
Wengine ambao aliwateua kuwa wabunge na kisha kuwateua kuwa mawaziri
ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano),
Balozi Dk Augustine Mahiga (Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki), Dk Philip Mpango (Fedha na Mipango), Profesa Joyce
Ndalichako (Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi), Dk
Abdallah Possi (Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Watu Wenye Ulemavu).
Mwingine ni Dk Tulia Ackson ambaye ni Naibu Spika wa Bunge. Kwa
upande wa wasifu wa Profesa Kabudi, ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam akiwa katika Bodi ya Uongozi inayotawala kuanzia
mwaka 2015 hadi 2018 akiwa na wadhifa wa Mwanasheria na Katibu wa Bodi
hiyo ya Uongozi.
Alikuwa Mjumbe wa Bunge la Katiba lililokaa na kupitisha Rasimu ya
Katiba Inayopendekezwa mwaka 2015, na amekuwa mmoja wa wasomi
wanaotegemewa katika nyanja mbalimbali nchini, lakini akiwa gwiji katika
masuala ya sheria.
Aidha, wasifu wa Profesa Kabudi unaonesha kuwa Julai 5, mwaka jana,
aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya TIB, lakini
akiwa pia na nyadhifa mbalimbali katika vyama vya kitaaluma na taasisi
za kidini.
Kwa upande wa Bulembo, mbali ya kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi
ya CCM Taifa ambayo inamfanya moja kwa moja kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na
Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho tawala, alikuwa miongoni mwa
wajumbe 32 wa Kamati ya Kumnadi mgombea wao wa urais mwaka 2015, Dk John
Magufuli, lakini akapewa jukumu la kuwa Mratibu akitembea na mgombea
huyo kwa muda wote wa kampeni iliyozaa ushindi wake Oktoba 25, 2015.
Kabla ya kuwa Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Bulembo alikuwa Mjumbe wa
Baraza Kuu la Utekelezaji la jumuiya hiyo, na ameshikilia nyadhifa
mbalimbali za uongozi kutoka katika ngazi za chini ikiwamo kuwa Diwani
wa Kata ya Nyasho katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara.
Aidha, Bulembo anafahamika kuwa mwanamichezo maarufu nchini, akiwahi
kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania
(FAT) katika miaka ya mwishoni mwa 1990, na pia kiongozi wa Chama cha
Soka Mkoa wa Mara (FAM). Mtoto wa Bulembo, Halima Bulembo pia ni Mbunge
CHANZO GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment