Na Ismail Ngayonga
MAELEZO
DAR ES SALAAM
KATIKA kufikia uchumi
wa kati ifikapo mwaka 2025, Serikali imekusudia kuweka mkazo katika
ujenzi vya viwanda ili kuharakisha kasi ya ukuaji wa maendeleo kwa
wananchi na taifa kwa ujumla.
Ili kufikia lengo
hilo, Serikali imeanisha sekta kuu za kiuchumi ikiwemo mifugo, uvuvi,
kilimo, ardhi, nishati, maji na kadhalika kuwa vipaumbele vikuu vya
kimkakati vilivyojengewa uwezo wa kutumia rasilimali na malighafi
ilizonazo hususani katika kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Idadi ya viwanda hapa
nchini imeendelea kuongezeka kutoka viwanda 125 Mwaka 1961 hadi kufikia
viwanda 54,422 mwaka 2016, Aidha, kati ya hivyo, viwanda vikubwa
vinavyoajiri kuanzia watu 100 ni 247, viwanda vya kati vinavyoajiri kati
ya watu 50 na 99 ni 170, viwanda vidogo vinavyoajiri kati ya watu
watano na 49 ni 6,907.
Kulingana na takwimu hizo, ni dhahiri kuwa
asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo sana na viwanda
vidogo, ambavyo hutegemea sekta zisizo rasmi katika kutengeneza ajira
za moja kwa moja kwa wananchi.
Uvuvi ni miongoni wa
shughuli kuu ya kiuchumi kwa wananchi wengi wanaozunguka maeneo ya
ukanda wa bahari, mito na maziwa, ambapo hutumia mazao ya rasilimali za
maji kwa ajili ya lishe na kujiongezea kipato.
Akizungumza hivi
karibuni Jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo
na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Yohana Budeba anasema Serikali imeanza mchakato
wa kuwahamisha wananchi kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya
mazao ya uvuvi nchini.
Dkt. Budeba anasema
hadi sasa jumla jumla ya viwanda vidogo vidogo 48 vya kuchakata samaki,
ambapo 36 vipo katika ukanda wa pwani, 11 ukanda wa ziwa Victoria na 1
ukanda wa ziwa Tanganyika, ambapo vyote kwa pamoja vimekusudia kuongeza
ajira na kuondoa umaskini kwa Watanzania.
“Mwaka 2015 jumla ya
tani 42,000 za samaki ziliuzwa na jumla ya Tsh. Bilioni 1.6 ziliweza
kukusanywa, hivyo tunaamini kuwa ujenzi wa viwanda utaweza kuiwezesha
sekta hii kuongeza mchango wake katika pato la taifa kutoka asilimia 2.4
ya sasa” anasema Budeba.
Dkt. Budeba anasema
Serikali imekusudia kujenga vituo vya kutotolesha samaki ili kuwezesha
Tanzania kuwa kuzalisha tani 50,000 za samaki katika kipindi cha miaka
mitano ijayo, ambapo kwa sasa Serikali ipo katika mazungumzo na Serikali
ya Japan kwa ajili ya kujenga vituo katika mikoa ya Tanga, Morogoro na
Rukwa.
Anaongeza kuwa kusudio
la ujenzi wa vituo hivyo ni pamoja na kuanzisha mpango wa uzalishaji wa
mbegu bora za samaki ikiwemo sato na sangara, ambao wamekuwa wakipendwa
na wananchi kwa ajili ya matumizi ya kitoweo ili kuchangia lishe bora.
Kwa mujibu wa Dkt.
Budeba anasema ili kuhakikisha wananchi wanafuga kwa kuzingatia kanuni
za ufugaji bora, Serikali imekusudia kusambaza Wataalamu katika kila
Kata nchini hatua inayolenga kuwajengea uwezo wafugaji kufuga kisasa
zaidi.
Akifafanua zaidi Dkt.
Budeba anasema Serikali itaendelea kuongeza idadi ya waatalamu wa uvuvi
nchini, ambapo imepanga kuzalisha na maafisa ugani 5000 kupitia vyuo vya
mafunzo ya uvuvi vya Mbegani- Bagamoyo, Nyegezi-Mwanza na Kigoma.
Aidha Budeba anasema
Serikali inaendelea kuwahamisha wafugaji kujiunga katika vyama vya
ushirika wa msingi vilivyopo katika Halmashauri, kwani kupitia vikundi
huweza kutoa mikopo na ruzuku mbalimbali.
“Mwaka 2015/16
Serikali ilitoa kiasi cha Tsh. Milioni 440 kwa vikundi 73 vya ushirika
wa wafugaji samaki, na pia ruzuku katika vifaa vya uvuvi na vyakula vya
samaki, na mashirika ya hifadhi ya jamii ikiwemo NSSF nao wameanza
utaratibu huu” anasema Budeba.
Akizungumzia kuhusu
shirika la Uvuvi Nchini (TAFICO), Dkt. Budeba anasema Serikali
imekusudia kurejesha hadhi ya shirika hilo, ambapo imepanga kununua meli
tano kubwa za kisasa ili kuliwezesha shirika hilo kufanya shughuli za
uvuvi katika maji ya kina kirefu.
Jitihada za Serikali
zinazoendelea kuelekezwa katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na
biashara na kuendeleza viwanda vidogo, zitasaidia wananchi walio wengi
zaidi kupata ajira, kuongeza kipato na kupunguza umasikini kupitia
uvuvi.
Uchumi wa viwanda
kupitia sekta ya uvuvi utaliweka taifa letu kuwa katika kundi la mataifa
yanayozalisha bidhaa bora na zenye ushindani wa soko la kimataifa
badala ya kuwa chanzo cha malighafi na soko la bidhaa kwa viwanda vya
mataifa mengine.
Ili kufikia azma hiyo,
ushirikiano na mchango wa mtu mmoja mmoja, makundi ya watu, taasisi za
umma na taasisi za binafsi utahitajika, hiyo ni pamoja na kila mmoja
wetu kwa uwezo wake kulenga kuwekeza katika viwanda vyetu na kupenda
kununua mazao ya samaki yanayozalishwa nchini.
MWISHO.
0 comments:
Post a Comment