Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
17/02/2017
Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema kuwa
hatua kali zitachukuliwa kwa atakayepokea rushwa kutoka kwa wauzaji,
wasambazaji na watumiaji wa Madawa ya Kulevya.
Ameyasema
hayo leo jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kikao cha kwanza
cha Baraza la Taifa la kudhibiti dawa za kulevya nchini.
“Sheria
ya udhibiti wa madawa ya kulevya itumike vizuri, Serikali na Baraza
halitahitaji mtu yeyote mwenye mamlaka kupokea rushwa ikigundulika hatua
kali zitachukuliwa” alifafanua Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri
Mkuu alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuendelea
kuimarisha mapambano dhidi ya udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini ambayo
yamekuwa yakifanywa na Serikali za Awamu zilizotangulia.
Aidha,
Waziri Mkuu alisema kuwa mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya ni vita
inayotakiwa kupigana kwa nguvu kubwa kwani madhara ya dawa hizo ni kubwa
kwa jamii hususani vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
“Tunahitaji
ushirikiano wa karibu wa pande zote mbili za Muungano kwani tatizo hili
limeathiri pande zote na ukanda wa bahari unatumika sana kama njia ya
kuingiza dawa hizo”
“Wakuu
wa Mikoa mna kazi kubwa katika vita hii, mkiwa wenyeviti wa Kamati za
Ulinzi na Usalama mpo kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa
mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo” alisema Waziri Mkuu.
Hata
hivyo Waziri Mkuu alibainisha kuwa, wajibu wa Baraza ni kusimamia
utekelezaji wa Sera ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini, ambapo jukumu
hilo ni kubwa na wajumbe wa Baraza hilo wanatakiwa kulitekeleza kwa
uadilifu na umahiri mkubwa.
Baraza
la Taifa la kudhibiti Dawa za Kulevya limeanzishwa chini ya kifungu cha
5 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya
mwaka 2015 ambapo Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na
wajumbe wengine wakiwemo Waziri anayeshughulikia Mambo ya Sheria, Waziri
anayeshughulikia Mambo ya Ndani ya Nchi.
Wengine
ni Waziri anayeshughulikia Afya, waziri anayeshughulikia Maendeleo ya
Jamii, Waziri anayeshughulikia Mambo ya Nchi za Nje, Waziri
anayeshughulikia Fedha, Waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Vijana,
Waziri anayeshughulikia Elimu, Waziri anayeshughulikia Kilimo, Waziri
anayeshughulikia Uchukuzi na Waziri anayeshughulikia Ulinzi.
0 comments:
Post a Comment