JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limethibitisha
kumshikilia mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji kwa mahojiano
baada ya kukutwa na jora 43 za sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa
Tanzania (JWTZ) pamoja na mihuri 39 ya kampuni tofauti tofauti.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda
Maalumu, Lucas Mkondya alisema Manji anashikiliwa na jeshi hilo tangu
Julai mosi baada ya kukutwa na vitu hivyo katika ghala lake la Quality
Motors, lililopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam.“Ni kweli tunamshikilia
tangu Jumamosi tunaendelea kumhoji kwa vitu alivyokutwa navyo ili
atuambie alivipataje na anavyo kwa madhumuni gani wakati yeye sio
mwanajeshi na amekaa navyo kwake,” alieleza Mkondya.
Akizungumzia endapo Manji atafikishwa mahakamani baada ya mahojiano,
Kaimu Kamanda Mkondya alisema baada ya kukamilisha mahojiano na kupata
taarifa kamili, wataangalia kama atapelekwa mahakamani kutokana na
majibu yake. “Tunasubiri tumalize mahojiano tupate na maelezo yake ili
tuone yamekwendaje na kama atafikishwa mahakamani kulingana na mahojiano
yatakavyokwenda,” aliongeza Mkondya.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Manji kushikiliwa na jeshi hilo kwa
mahojiano. Februari mwaka huu, Manji aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa
Quality Group kabla ya kustaafu Julai mwaka jana, alishikiliwa kwa
mahojiano baada ya kudaiwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.
Katika hatua nyingine, Manji na wenzake wamepeleka maombi Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, kuomba Jeshi la Polisi kuwaachia huru kwa kuwa
wanashikiliwa isivyo halali kwa tuhuma zinazohusiana na sare za JWTZ.
Aidha, wameomba mahakama itoe amri kwa jeshi hilo kuwataka wawapeleke
waombaji mahakamani washughulikiwe kwa mujibu wa sheria. Mbali na
Manji, waombaji wengine katika kesi hiyo ni Deogratius Kisinda na
Thobias Fwere ambao wamewasilisha maombi hayo dhidi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali (AG), Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) na Mkuu wa
Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZCO).
Katika hati ya kiapo iliyoungwa mkono na maombi hayo, Wakili wa
washitakiwa, Hudson Ndusyepo alidai walalamikaji walikamatwa na
kushikiliwa na ZCO kwa nyakati tofauti; Kisinda alikamatwa Juni 30,
mwaka huu saa 10 jioni wakati Manji na Fwere walikamatwa Julai mosi saa 5
katika Jengo la Quality Center, Barabara ya Nyerere.
Ndusyepo alidai kuwa tangu siku hiyo mpaka sasa, walalamikaji
wanashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi na kwamba alifahamishwa na
ZCO kuwa walikamatwa kwa tuhuma za kutenda kosa linalohusiana na sare
zilizokutwa kwenye stoo ya Quality Motors Limited. Pia alidai baada ya
kukamatwa kwa walalamikaji hao, aliwaombea dhamana, lakini maombi hayo
yalikataliwa kwa sababu zisizojulikana ambapo walikuwa wakifuatilia
dhamana za waombaji tangu walipokamatwa.
CHANZO HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment